• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
‘Azimio kupoteza viti vikuu kutokana na ushindani miongoni mwa vyama tanzu’

‘Azimio kupoteza viti vikuu kutokana na ushindani miongoni mwa vyama tanzu’

Na CHARLES WASONGA

MUUNGANO wa Azimio La Umoja-One Kenya unakabiliwa na hatari ya kupoteza viti mbalimbali katika uchaguzi mkuu ujao kutokana na ushindani kati ya wawaniaji wa vyama tanzu ndani yake.

Hii ni baada ya vyama hivyo kupinga pendekezo la uongozi wa muungano kutenga maeneo fulani wakilishi – zoning – kwa wawaniaji watakaobainika kuwa maarufu.

Mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga, Jumatano wiki jana alisema muungano huo utaendesha kura ya maoni kubaini wawaniaji wa vyama tanzu katika Azimio ambao ni maarufu. Kisha wale ambao watabainika kuwa dhaifu watashauriwa kujiondoa na kuunga mkono wenzao maarufu.

“Katika maeneo ambako tuko na wawaniaji waliodhaminiwa na vyama vilivyoko ndani ya Azimio, tumekubaliana kwamba watafanya kampeni kwa mwezi mmoja kisha tutafanya kura ya maoni,” Bw Odinga akasema Jumatano katika mkahawa mmoja mjini Thika alipokutana na wafuasi wa Azimio kutoka Murang’a.

“Wale ambao itabainika ni dhaifu watashauriwa kujiondoa ili tusigawanye kura na kushindwa na wapinzani wetu,” akaongeza.

Tangazo hilo lilitolewa kwa msingi wa ripoti moja iliyoandaliwa na kamati ya kiufundi iliyopendekeza vyama fulani vitengewe maeneo fulani wakilishi ili kuzuia hatari ya Azimio kupoteza viti muhimu katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Ripoti hiyo ilitambua maeneo ambako Azimio ni maarufu lakini inakabiliwa na hatari ya kupoteza kwa muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto wa chama maarufu kwa mujibu wa kura za maoni, cha United Democratic Alliance (UDA).

Hii ndio maana katika kinyang’anyiro cha ugavana Azimio inalenga kuwa na mgombeaji mmoja katika kaunti za Kisii, Nyamira, Mombasa, Kakamega na Wajir.

Katika kaunti ya Kisii, kiti cha ugavana kimevutia wagombeaji wafuatao; Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Simba Arati anayewania kwa tiketi ya ODM, Profesa Sam Ongeri (DAP-K), Chris Obure (Jubilee).

Wote hawa watashindana na Ezekiel Machogu ambaye amedhaminiwa na UDA.

Katika kaunti ya Kakamega Mbunge wa Lugari Ayub Savula (DAP-K), aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya stima ya Ketraco Fernandes Barasa (ODM) na mbunge wa Shinyalu Justus Kizito (UDP), wote ni wanachama wa Azimio wanang’ang’ania ugavana.

Watashindana na Cleophas Malala wa ANC ambaye anapeperusha bendera ya Kenya Kwanza.

Katika kaunti ya Nyamira Azimio imewasilisha gavana wa sasa Amos Nyaribo ambaye anatetea kiti hicho kwa tiketi ya chama cha United Progressive Alliance (UPA), Timothy Bosire (ODM), mbunge wa Borabu Ben Momanyi (Wiper) na Mwancha Okioma (Jubilee).

Wawaniaji hao wanne wa Azimio watakabiliana na mgombeaji wa Kenya Kwanza Walter Nyambati (UDA).

Muungano wa Azimio pia unakabiliwa na kizungumkuti kingine katika kaunti ya Wajir ambako ODM imedhamini gavana wa zamani Ahmed Abdullahi, Siyad Abdullahi Ugass Sheikh (PNU), Mohamed Elmi (Jubilee).

Wagombeaji hawa wanatarajiwa kupambana na Naibu Gavana Ahmed Muktar ambaye amedhaminiwa na UDA.

Licha ya Azimio kukabiliwa na hatari ya kupoteza viti hivi vya ugavana wa Kisii, Nyamira, Kakamega na Wajir maafisa wa vyama tanzu wanashikilia kuwa sharti wawaniaji wao waruhusiwe kushiriki.

Bw Savula, ambaye ni naibu kiongozi wa DAP-K anasisitiza kuwa ni kinyume ya misingi ya kidemokrasia ikiwa yeye na wawaniaji wengine wa chama hicho wataagizwa kujiondoa ili wawapishe wenzao wa vyama vikubwa kama ODM.

“Binafsi naelekea hadi debeni katika azma yangu ya kuwa gavana wa Kakamega. Wapigakura wa Kakamega sharti wapewe nafasi ya kuamua ni nani atakuwa gavana wao,” akasema.

Naye Katibu Mkuu wa DAP-K Simiyu Eseli amesema kuwa watapinga jaribio lolote la kuwalazimisha kumwondoa Profesa Ongeri kutoka kinyang’anyiro cha ugavana Kisii.

Kwa upande mwingine, Katibu Mkuu wa chama cha United Democratic Movement (UDM) David Ohito, ameshikilia kuwa hakiondoi wawaniaji katika kaunti ya Siaya.

“Tumewasilisha majina ya wawaniaji wetu kwa IEBC na tutawatetea hadi wafike debeni,” akasema Bw Ohito.

UDM kinachoongozwa na Gavana wa Mandera Ali Roba kimedhamini aliyekuwa mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo kuwania ugavana wa Siaya dhidi ya mgombeaji wa ODM seneta James Orengo. Aidha, chama hicho kimedhamini Nero Adhola kuwania kiti cha ubunge cha Rarieda na Fredrick Dor katika eneobunge la Ugunja.

Bw Ohito amepinga pendekezo kwamba UDM kiondoe wawaniaji wake Siaya ili kuwapisha wawaniaji wa ODM akisema hamna hatari yoyote ya Azimio kupoteza viti katika kaunti hiyo.

“Hamna hatari ya kura za Azimio kugawanyika Siaya kwa sababu hamna wagombeaji wa UDA katika kaunti hii. Vyama vingine katika Kenya Kwanza pia havina uwezo wa kushinda kiti chochote katika kaunti hii,” Bw Ohito akaeleza.

Katibu huyo mkuu alisema uwepo wa wawaniaji wa UDM na vyama vingine katika Azimio katika kinyang’anyiro cha viti uchaguzi wa Agosti utavutia idadi kubwa ya wapigakura kujitokeza.

“Hali hii itamfaidi mgombea urais wa Azimio Raila Odinga kwa sababu kura zote za urais zitaingia kwenye kapu lake,” Bw Ohito akaeleza.

Lakini Katibu Mkuu wa Jubilee anasema ipo haja ya kuwepo kwa maelewano ndani ya Azimio ili muugano huo uweze kushinda viti vingi katika Seneti na Bunge la Kitaifa.

“Mahala popote ambapo tutahisi kuwa kutatokea ushindani mkali miongoni mwa vyama vyetu na hivyo kuchangia wawaniaji wetu kupoteza, tutatumia maelewano kuhakikisha kuwa Azimio inapata viti tosha bungeni,” Jeremiah Kioni, ambaye ni mbunge wa Ndaragua, akaongeza.

  • Tags

You can share this post!

Man-City waponda Newcastle United ugani Etihad na kurejea...

Urusi yadaiwa kuua 60 kwa bomu katika shule

T L