• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Man-United na Chelsea nguvu sawa katika gozi la EPL ugani Old Trafford

Man-United na Chelsea nguvu sawa katika gozi la EPL ugani Old Trafford

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao na kuvunia waajiri wake Manchester United alama moja baada ya sare ya 1-1 dhidi ya Chelsea katika gozi kali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Alhamisi usiku ugani Old Trafford.

Chelsea walitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira katika vipindi vyote viwili vya mchezo. Hata hivyo, makali yao yalidhibitiwa vilivyo na kipa David de Gea aliyepangua makombora mazito aliyoelekezewa na Kai Havertz, Timo Werner na N’Golo Kante.

Chelsea walijiweka kifua mbele katika dakika ya 60 kupitia kwa Marcos Alonso kabla ya Ronaldo kusawazisha mambo dakika mbili baadaye.

Bao la Ronaldo ambaye sasa anafukuzia taji la mfungaji bora wa EPL msimu huu lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo mkabaji Nemanja Matic. Ronaldo angalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili ila akazidiwa ujanja na kipa Edouard Mendy.

Chelsea nao walipoteza nafasi nyingi za kufunga magoli zaidi kupitia kwa Reece James aliyeshuhudia mojawapo ya makombora yake yakibusu mhimili wa lango la Man-United.

Matokeo hayo yaliweka hai matumaini ya Chelsea ya kocha Thomas Tuchel kukamilisha kampeni za EPL muhula huu ndani ya orodha ya nne-bora. Kufikia sasa, Chelsea wanashikilia nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 66, sita zaidi kuliko Arsenal wanaokamata mduara wa nne-bora.

Man-United kwa upande wao wanashikilia nafasi ya sita kwa pointi 55, tatu nyuma ya nambari tano Tottenham Hotspur. Licha ya matumaini ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya nne-bora kuyeyuka, kocha mshikilizi Ralf Rangnick ametaka waajiri wake Man-United kufunga msimu kwa matao ya juu na kushinda mechi zote tatu walizosalia nazo muhula huu.

Chelsea walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kunyanyasa Man-United ikizingatiwa kwamba walikuwa wameshinda mechi nane za awali ugenini katika mashindano yote.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ashuu ashusha pumzi kwa muda

Ralf Rangnick apokezwa mikoba ya timu ya taifa ya Austria

T L