• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Man-United watia kocha Nuno katika hatari ya kupigwa kalamu na Spurs

Man-United watia kocha Nuno katika hatari ya kupigwa kalamu na Spurs

Na MASHIRIKA

KIUNGO Pierre-Emile Hojbjerg wa Tottenham Hotspur amesema matokeo ya timu yao katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyowapa Manchester United jukwaa la kuwatandika 3-0 mbele ya mashabiki wa nyumbani mnamo Jumamosi “hayakubaliki kabisa”.

Ingawa Spurs kwa sasa wako ndani ya mduara wa 10-bora katika msimamo wa jedwali la EPL, kikosi hicho cha kocha Nuno Espirito Santo kimefunga mabao tisa pekee kutokana na mechi 10 zilizopita ligini na kilishindwa kabisa kufyatua kombora lolote lililolenga shabaha langoni mwa Man-United.

“Kucheza jinsi tulivyofanya dhidi ya Man-United hakukubaliki. Kila mmoja alitarajia fataki kulipuka na kikosi kutandaza boli kwa kujituma zaidi mbele ya mashabiki wa nyumbani. Lakini mambo yalituendea kombo katika kila idara. Tulitepetea na wageni wakatutamalaki,” akasema nyota huyo raia wa Denmark.

Huku kichapo kikimning’iniza padogo kocha Nuno kambini mwa Spurs, mabao matatu ambayo Man-United walifunga kupitia Cristiano Ronaldo, Edinson Cavani na Marcus Rashford yalikuwa kitulizo kikubwa kwa kocha Ole Gunnar Solskjaer aliyekuwa akikabiliwa na presha ya kupigwa kalamu ugani Old Trafford kwa sababu ya matokeo duni.

Man-United walijitosa ulingoni wakiwa na kiu ya kujitoa topeni baada ya kupigwa na Leicester City (4-2) na Liverpool (5-0) ligini. Ushindi dhidi ya Spurs ulikuwa wao wa kwanza baada ya mechi tano za EPL na kwa sasa wanajivunia alama 17 sawa na Arsenal. Japo ufanisi huo ni afueni kwa ‘mashetani wekundu’ wa Man-United, mabingwa hao mara 20 wa EPL wangali na ratiba ngumu katika kipindi cha mwezi mmoja ujao.

Baada ya kurudiana na Atalanta ya Italia kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) hapo kesho ugenini, masogora wa Solskjaer watachuana na Manchester City na Watford ligini kabla ya kukwaruzana tena na Villarreal katika soka ya bara Ulaya. Watafunga kampeni za Novemba na kufungua Disemba kwa vibarua vizito vya EPL dhidi ya Chelsea, Arsenal na Crystal Palace mtawalia.

Ingawa hivyo, sasa joto la kuwa kocha wa tatu kutimuliwa katika EPL msimu huu baada ya Xisco Munoz (Watford) na Steve Bruce (Newcastle United) linamfuata Nuno. Mkufunzi huyo alikubali kuwa mrithi wa Mreno mwenzake, Jose Mourinho, kambini mwa Spurs muhula huu baada ya kuagana rasmi na Wolverhampton Wanderers mwishoni mwa msimu 2020-21.

Nuno ndiye mkufunzi wa kwanza wa Spurs baada ya Christian Gross mnamo 1997-98 kuwahi kupoteza mechi tano kati ya 10 za ufunguzi wa msimu kwenye kampeni za EPL.

Isitoshe, tofauti ya mabao inayojivuniwa na Spurs (-7) ndiyo ya chini zaidi kuliko ya vikosi vyote vingine nje ya mduara unaojumuisha klabu tatu za mwisho jedwalini. Ni Norwich City pekee ambao wamefunga idadi ndogo zaidi ya mabao ya EPL kufikia sasa msimu huu.

Wanasoka wa Spurs waliondoka katika uga wao wa nyumbani wakiinamisha vichwa kwa aibu huku wakizomewa na mashabiki ambao awali, walimchemkia Nuno kwa hatua ya kumwondoa uwanjani fowadi Lucas Moura na mahali pake kuchukuliwa na Steven Bergwijn.

“Huo ndio uhalisia. Kikosi kisiposajili matokeo ya kuridhisha, mashabiki ndio huwa wa kwanza kukasirika. Hata hivyo, tunawaomba waendelee kutuunga mkono kwa sababu hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuboresha mambo,” akatanguliza Nuno.

“Tulianza mchuano huo vyema. Vijana walijituma vilivyo lakini tukapoteza dira mwanzoni mwa kipindi cha pili na motisha ikapotea kabisa baada ya Man-United kutufunga bao la pili. Ipo fursa nyingine ya kujirekebisha na ninaamini tutafufua makali yetu,” akaongeza.

Spurs ambao kwa sasa wamefungwa mabao 16 ligini, walishuka dimbani wakitarajiwa kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa 1-0 na West Ham United katika mechi ya awali ya EPL. Masogora hao wa Nuno walianza kampeni za ligi muhula huu kwa kukung’uta mabingwa watetezi Man-City 1-0 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Wolves na Watford.

Kabla ya kujinyanyua na kucharaza Aston Villa (2-1) na Newcastle United (3-2), Spurs walikuwa wamekomolewa na Palace (3-0), Chelsea (3-0) na Arsenal (3-1). Kwa sasa wanakabiliwa na kibarua kigumu cha kunyanyasa Vitesse ya Ligi Kuu ya Uholanzi kwenye Europa League mnamo Alhamisi kabla ya kurejelea kampeni za EPL kwa mechi dhidi ya Everton na Leeds United kwa usanjari huo.

You can share this post!

Brighton watoka nyuma na kubana Liverpool ligini

Chelsea wafungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali...

T L