• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 3:09 PM
Chelsea wafungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la EPL

Chelsea wafungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

REECE James alifunga mabao mawili na kusaidia Chelsea kufungua pengo la alama tatu kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kucharaza Newcastle United 3-0 uwanjani St James’s Park mnamo Jumamosi.

James alijaza kimiani krosi aliyopokezwa na Callum Hudson-Odoi katika dakika ya 65 na kuweka Chelsea kifua mbele kabla ya beki huyo kumzidi maarifa kipa Karl Darlow kwa mara nyingine katika dakika ya 77 baada ya kushirikiana na Ruben Loftus-Cheek.

Darlow alimkabili visivyo fowadi Kai Havertz mwishoni mwa kipindi cha pili na kusababisha penalti ambayo Chelsea walifungiwa na Jorginho. Newcastle waliokuwa wakichezea nyumbani kwa mara ya kwanza tangu kocha Steve Bruce apigwe kalamu, walijituma vilivyo katika kipindi cha kwanza ila bahati haikusimama nao baada ya kombora la Callum Wilson kugonga mwamba wa goli la Chelsea.

Matokeo hayo yaliendeleza masaibu ya Newcastle ambao hawajashinda mechi yoyote kufikia sasa ligini msimu huu. Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea walifungua mwanya huo wa pointi tatu baada ya wapinzani wao wakuu kwenye EPL msimu huu kujikwaa katika michuano yao.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp iliambulia sare ya 2-2 dhidi ya Brighton ugani Anfield nao mabingwa watetezi Manchester City wakatandikwa 2-0 na Crystal Palace ugani Etihad. Jumla ya mashabiki 52,209 walifika uwanjani St James’ Park kushuhudia mechi ya pili ya Newcastle tangu umiliki wa kikosi hicho utwaliwe na mabwanyenye wa Saudi Arabia kwa Sh48 bilioni.

Ilikuwa mechi ya kwanza kwa kocha mshikilizi Graeme Jones kusimamia kambini mwa Newcastle tangu waagane na Bruce mwanzoni mwa mwezi Oktoba 2021. Newcastle walisalia imara katika kipindi chote cha kwanza huku kukosekana kwa wavamizi Romelu Lukaku, Timo Werner na Mason Mount kukihisika pakubwa kambini mwa Chelsea.

Hakim Ziyech, Antonio Rudiger na Havertz walipoteza nafasi nyingi za wazi ambazo vinginevyo, zingewaweka Chelsea kifua mbele katika kipindi cha kwanza. Newcastle kwa sasa wanakamata nafasi ya 19 jedwalini kwa alama nne, mbili zaidi kuliko Norwich City wanaovuta mkia.

You can share this post!

Man-United watia kocha Nuno katika hatari ya kupigwa kalamu...

Crystal Palace waduwaza Man-City kwenye EPL

T L