• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 2:31 PM
Mandonga ‘Mtu Kazi’ amlipua Wanyonyi kwa ngumi za TKO

Mandonga ‘Mtu Kazi’ amlipua Wanyonyi kwa ngumi za TKO

NA CHARLES ONGADI

HATIMAYE bondia mwenye tambo na vitisho kibao Karim ‘Mtu Kazi’ Mandonga kutoka Tanzania, amedhihirisha vitendo ulingoni baada ya kumuangusha Daniel Wanyonyi kwa njia ya TKO (Technical Knock Out).

Pigano hilo la uzito wa Supermiddle liliandaliwa katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi mnamo Jumamosi usiku.
Awali liliratibiwa kuwa la “kufungua pazia” kusapoti pigano kuu la siku kati ya Mkenya Rayton ‘Boom Boom’ Okwiri na Ally Shabani Ndaro pia wa Tanzania.

Hata hivyo, kutokana na gumzo kuu miongoni mwa mashabiki nchini na Tanzania hasa mitandaoni, pigano lililibadilishwa dakika za lala salama kuwa pigano kuu.

Mandonga alianza kwa kumsoma makini Wanyonyi, ambaye ni bingwa wa zamani wa taji la Afica Boxing Union (ABU), aliyeonekana kutokuwa na haraka.

Lakini kadri muda ulivyoyoyoma ndivyo Mandonga alipata motisha na kuzidisha makombora dhidi ya Wanyonyi aliyejibu kwa ngumi za kushtukiza.

Hata hivyo, ilipofika raundi ya tano Wanyonyi alionekana kukosa dira akijikunja kila mara na kukosa kujibu mipigo ya ‘Mtu Kazi’.

Katika raundi ya tano, Mkenya huyo alionekana kuishiwa pumzi ya kuendelea kuzichapa huku Mandonga akinogesha mashambulizi yake kwa mtindo wa kutokea Ukraine, maarufu kama ‘ Sungunyo’.

Raundi ya sita ilipoanza, Wanyonyi alidinda kuendelea na mpambano akikataa kuondoka katika kona yake; ishara ya kutoweza kuendelea, ikamlazimu refa Julius Odhaimbo kuingilia kati kusimamisha pigano hili.

“Nawashukuru mashabiki wangu ukanda huu hasa hapa Kenya kwa sapoti yao. Nimejisikia niko nyumbani na imekuwa shwari,” akasema Mandonga mara baada ya kutawazwa mshindi.

Kwa upande wake, Okwiri alikabiliana kufa kupona dhidi ya Ndaro kinyume na ilivyotarajiwa, kabla kutawazwa mshindi kwa alama 80-72,80-72 na 79-73.

Aidha, ushindi huo umeimarisha rekodi ya Okwiri ya ushindi mara tisa — sita kwa njia ya KO — katika mapigano 11 ambayo ameshiriki.

Ameshindwa mara moja na kutoka sare moja.

Mapigano mengine Jumamosi hiyo yalikuwa kama ifuatavyo: James Nyariki (Kenya) alishindwa na Louis Cedrick Olivier (Mauritius) katika uzito wa Heavy; Lucien Botumbe (DRC) akamnyuka Adel Motean (Mauritius) kwa njia ya KO katika Supermiddle.

Upande wa akina dada, Praxides Anyango alimshinda Jane Kavulani katika uzito wa Feather.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto anavyotumia miradi ya maendeleo kama chambo...

Man-United waangusha City na kutawala gozi kali la...

T L