• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Man-United waangusha City na kutawala gozi kali la Manchester Debi kwa mabao 2-1

Man-United waangusha City na kutawala gozi kali la Manchester Debi kwa mabao 2-1

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Manchester City, walipoteza fursa ya kuendeleza presha kali kwa Arsenal kileleni mwa jedwali la kipute hicho baada ya watani wao Manchester United kuwapokeza kichapo cha 2-1 ugani Old Trafford.

Man-United wanaojivunia ufufuo mkubwa wa makali yao walitoka nyuma na kusawazisha kupitia kwa Bruno Fernandes katika dakika ya 78 kabla ya Marcus Rashford kuwafungia bao la ushindi dakika nne baadaye. Man-City walipata goli lao kupitia kwa Jack Grealish kunako dakika ya 60.

Matokeo hayo yalipaisha masogora wa kocha Erik ten Hag hadi nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 38, sita nyuma ya Arsenal watakaomenyana na Tottenham Hotspur mnamo Januari 15, 2022.

Man-United walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kulipiza kisasi dhidi ya majirani waliowadhalilisha kwa mabao 6-3 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa EPL mnamo Oktoba 2022 ugani Etihad.

Tangu Man-United wapokezwe kichapo hicho na Man-City, wamepoteza mechi moja pekee kati ya 19. Aston Villa iliwatandika 3-1 mwanzoni mwa Novemba 2022 na wameshinda mechi saba mfululizo tangu fainali za Kombe la Dunia zikamilike nchini Qatar.

Hadi walipovaana na Man-City, walikuwa wamekomoa Charlton 3-0 katika nusu-fainali ya Carabao Cup mnamo Jumanne kupitia kwa mabao ya Antony dos Santos na Marcus Rashford ambaye sasa anajivunia magoli manane ligini muhula huu.

Ten Hag ameongoza sasa waajiri wake kushinda mechi 21 kutokana na 28, akiweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza katika historia ya Man-United kufikia hatua hiyo ya ufanisi baada ya michuano michache zaidi. Matokeo dhidi ya Man-City yanaweka hai matumaini ya mabingwa hao mara 20 wa EPL kutia kapuni mataji manne msimu huu wa 2022-23 kadri wanavyofukuzia pia ufalme wa Europa League, Carabao Cup na Kombe la FA.

Man-United wamejizolea alama nyingi zaidi kuliko kikosi chochote kingine chochote cha EPL (38) tangu wapige Liverpool 2-1 mnamo Agosti 22, 2022. Wameshinda jumla ya mechi 12 kati ya 16 katika kipindi hicho, 10 zikiwa katika uga wao wa nyumbani.

Kinyang’anyiro dhidi ya Man-City kilikuwa kipimo halisi cha uthabiti wao ikizingatiwa kwamba walikuwa awali wamepoteza mechi tatu mfululizo dhidi ya masogora hao wa kocha Pep Guardiola kwa jumla ya mabao 12-4. Man-City walitarajiwa kujinyanyua upesi baaada ya kudenguliwa na Southampton kwenye robo-fainali ya Carabao Cup mnamo Jumatano usiku ugani St Mary’s.

Mechi dhidi ya Man-United ilikuwa ya 500 kwa Guardiola kusimamia katika historia yake ya ukufunzi na ya 246 akidhibiti mikoba ya Man-City waliosalia katika nafasi ya pili jedwalini kwa alama 39, nane nyuma ya Arsenal waliopiga Spurs katika gozi la 193 la London Kaskazini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mandonga ‘Mtu Kazi’ amlipua Wanyonyi kwa ngumi za TKO

TALANTA YANGU: Keycee ndiye Messi wa kesho

T L