• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Rais Ruto anavyotumia miradi ya maendeleo kama chambo kunasa ngome za Raila

Rais Ruto anavyotumia miradi ya maendeleo kama chambo kunasa ngome za Raila

NA CHARLES WASONGA

MIRADI ya maendeleo ambayo Rais William Ruto amekuwa akiahidi kutekeleza katika ngome za kiongozi wa upinzani Raila Odinga inaonekana kama mbinu zake za kumdhibiti mwanasiasa huyo.

Tangu alipoingia mamlakani Septemba 13, 2022 Dkt Ruto amekuwa akifanya ziara katika maeneo ya Ukambani, Pwani, Magharibi na Nyanza akiahidi serikali yake itatekeleza miradi kadha ya kuchochea maendeleo katika maeneo hayo.

Hii ni licha ya kwamba wakazi wa maeneo hayo walimpa kura nyingi Bw Odinga, ambaye alikuwa mpinzani wake mkuu, katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

Wadadisi wanasema ziara za Dkt Ruto na “minofu ya maendeleo” anayotoa kwa wakazi ni sehemu ya mikakati yake ya kuwatia viongozi na wakazi upande wake kwa manufaa yake kisiasa, kuelekea 2027.

Tangu mwishoni mwa mwaka jana, Bw Odinga amekuwa akisisitiza kuwa serikali ya Kenya Kwanza haifai kubagua Ukambani, Pwani, Magharibi na Nyanza, kimaendeleo kwa misingi ya kuwa ngome cha Azimio la Umoja-One Kenya.

“Ni wajibu wa serikali iliyoko mamlakani kusambaza maendeleo katika sehemu zote za nchini, zikiwemo ngome zetu kama Azimio. Wafuasi wetu hawafai kuadhibiwa kwa kunyimwa maendeleo eti kwa sababu walinipigia kura ilhali wao pia ni walipa ushuru. Tutaendelea kupigania maendeleo kwa watu wetu katika msururu wa mikutano tutakayofanya katika ngome zetu za Magharibi, Pwani, Ukambani na Nyanza siku zijazo,” akasema alipohutubia wafuasi wa Azimio katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi, Desemba 7,2022.

Lakini mkutano wake kwanza wa Novemba 11, 2022, Baraza la Mawaziri chini ya uongozi wa Rais Ruto liliidhinisha ujenzi wa taasisi ya utafiti kuhusu rasilimali za samaki katika kaunti ya Kisumu.

Ujenzi wa taasisi hiyo itakayojulikana kama “Kabonyo Fisheries Aquaculture Service and Training Centre of Excellence” utagharimu Sh1 bilioni.

“Baraza la Mawaziri limeidhinisha kuanzisha kwa taasisi ya Kabonyo Fisheries Aquaculture Service and Training Centre of Excellence katika kaunti ya Kisumu. Tasisi hiyo itakayogharimu zaidi ya Sh1 bilioni itafanikisha mafunzo, utafiti, uvumbuzi na uendelezi wa mbinu bora za katika ufugaji samaki,” ikasema taarifa kutoka Ikulu ya Nairobi baada ya mkutano huo.

Mradi huo unatarajiwa kuwafaidi wakazi wa eneo zima la Nyanza ikizingatiwa kuwa wengi wao wanategemea uvuvi kama kitega uchumi.

Isitoshe, wiki hii Rais Ruto alifanya ziara ya kimaendeleo katika kaunti za Homa Bay, Kisumu na Siaya ambako aliahidi kuwa serikali yake itatekeleza miradi kadha ya kuwafaidi wakazi.

Katika kaunti Homa Bay, kiongozi wa Ruto alizindua mradi wa nyumba za 5,000 za gharama nafuu mjini Homa Bay.

Aidha, Rais Ruto aliahidi kuwa serikali itajenga soko kubwa la samaki kwa gharama ya Sh600 milioni mjini Homa Bay. Soko hilo pia litakuwa na kiwanda cha kutayarisha samaki.

“Samaki kutoka hapa Ziwa Victoria inafaa kuuzwa hapa ili kufaidi wakazi wa hapa. Hii ndio maana tunataka kujenga soko kubwa na kiwanda cha kuongeza thamani,” Dkt Ruto akaeleza, akifafanua kuwa serikali yake itafanikisha miradi hiyo “licha ya kwamba nilipata kura chache zaidi kutoka eneo hili.”

Aidha, kiongozi wa taifa aliahidi kuwa serikali ya itakamilisha miradi ya ujenzi wa barabara kadhaa zilizokwama katika kaunti hiyo.

Katika kaunti jirani ya Kisii, Gavana Simba Arati ametangaza kuwa Serikali ya Rais Ruto itasaidia katika utekelezaji mradi wa kiafya wa thamani ya Sh500 bilioni.

“Watu wengi wanajiuliza kwa nini nilienda Ikulu. Lakini nilienda kusaka baraka za Rais kwa mradi mkubwa utakaoanzishwa katika kaunti yangu. Mradi huo unalenga kuimarisha sekta ya afya katika kaunti ya Kisii na Serikali ya Uingereza iko tayari kuwekeza Sh500 bilioni kuufanikisha kwa ushirikiano na serikali kuu,” Bw Arati akasema mnamo Desemba 20, 2022.

Mnamo Desemba 2022, Rais Ruto alizindua mpango wa ujenzi wa nyumba 5,300 za gharama nafuu katika eneo la Syokimau, kaunti ya Machakos.

Dkt Ruto alifichua kuwa mradi huo utakaogharimu Sh20 bilioni utafadhiliwa na Serikali Kuu kwa ushirikiano na serikali ya kaunti na wadau wengine katika sekta ya kibinafsi.

“Mradi huu wa ‘Mavoko Housing Project’ utatoa ajira kwa vijana wetu na wakazi wa eneo hili kwa ujumla. Naamuru kwamba vifaa na malighafi yote yatakatumika katika mradi huu yanunuliwe kutoka kwa watu wa hapa ili wafaidi,” akasema.

Katika ziara aliyofanya Mombasa mwishoni mwa Desemba, mwaka jana Rais Ruto aliamuru kukamilishwa kwa mradi wa eneo la kiuchumi la Dongo Kundu wa thamani ya Sh39 bilioni. Mradi huo ni nguzo kuu katika ufanisi mwa mradi mpana wa Ustawishaji wa Bandari ya Mombasa.

Kiongozi wa taifa aliamuru kwamba mradi huo ukamilishwe kabla ya 2025 ili utoe ajira kwa vijana, haswa katika sekta ya viwanda vya kutengeza bidhaa kutokana na mazao ya shambani.

Aidha, wiki hii, Rais aliahidi kuwa Wizara ya Ardhi itaanzisha mpango kugeuza rekodi ardhi katika kaunti ya Mombasa kuwa katika mfumo wa kidijitali.

Akiongea katika Ikulu ya Nairobi alipotembelewa na Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sheriff Nassir, Dkt Ruto alisema mpango huo utaendeleza katika kaunti zote za Pwani ili kusuluhisha makosa ya kihistoria kuhusu umiliki wa ardhi eneo hilo.

Katika kaunti ya Kakamega, Rais Ruto ameahidi kuwa serikali yake itapanua uwanja wa ndege wa Kakamega ili ivutia ndege kubwa.

Akiongea katika Ikulu ndogo ya Kakamega mnamo Desemba 22, 2022, Dkt Ruto pia aliahidi kuwa serikali itafutilia mbali madeni yanayodaiwa kampuni za sukari za Mumias na Nzoia.

Aidha, kiongozi wa taifa aliahidi kutafuta mwekezaji mpya atakaendesha kampuni ya Mumias baada ya viongozi na wakazi kulalamikia utendakazi wa kampuni ya Sarrai Group kutoka Uganda iliyopewa usimamizi wa kampuni hiyo mwaka 2022.

  • Tags

You can share this post!

Spika wa Bunge la Kericho Patrick Mutai mashakani baada ya...

Mandonga ‘Mtu Kazi’ amlipua Wanyonyi kwa ngumi za TKO

T L