• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 3:46 PM
Martial ataka aachiliwe na Man-United atafute hifadhi mpya kwingineko

Martial ataka aachiliwe na Man-United atafute hifadhi mpya kwingineko

WAKALA wa Anthony Martial amesema fowadi huyo raia wa Ufaransa amewasilisha ombi la kutaka kuachiliwa na Manchester United ili atafute hifadhi mpya ya kitaaluma kwingineko wakati wa muhula mfupi wa uhamisho wa wachezaji mwezi ujao.

Martial, 26, amewajibishwa katika kikosi cha Man-United mara mbili pekee kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu na akafunga bao moja.

Isitoshe, hajachezeshwa katika mechi zozote ambazo zimesimamiwa na kocha mshikilizi Ralf Rangnick ambaye ameshikilia kuwa Martial anauguza jeraha alilopata mazoezini wiki iliyopita.

“Martial angependa kubanduka kambini mwa Man-United mnamo Januari. Anachokitamani zaidi ni fursa ya kucheza na asingetaka kusalia Man-United mwaka ujao. Nitazungumza na waajiri wake hivi karibuni ili tujadili mustakabali wake,” akasema Philippe Lamboley ambaye ni ajenti wa Martial.

Kabla ya kuongoza kikosi chake kuvaana na Norwich City ugani Carrow Road mnamo Disemba 11, Rangnick alifichua mpango wa kuzungumzia wachezaji wanaohisi kwamba wanakosa nafasi ya kuwajibishwa ipasavyo na Man-United ili kushawishi baadhi yao kujiunga na vikosi vingine kwa mkopo mnamo Januari.

Mkufunzi huyo raia wa Ujerumani pia alifichua kwamba alizumgumza na kiungo Paul Pogba kwa dakika 15 kupitia simu na wakaweka miadi ya kukutana uso kwa uso hii leo kujadili uwezekano wa kurefushwa kwa mkataba wake unaotamatika mwisho mwa msimu huu.

Pogba anatarajiwa kurejea Uingereza kutoka Dubai alikoelekea baada ya kupata jeraha la paja akishiriki mazoezi na timu ya taifa ya Ufaransa mwezi uliopita.

“Anaendelea vyema na atahitaji takriban wiki nne zaidi kabla ya kurejelea mazoezi mazito uwanjani na kuanza tena kuwajibikia Man-United,” akasema Rangnick.

You can share this post!

Haaland kuagana na Dortmund mwisho wa msimu huu wa 2021-22

Mahakama yasimamisha mazishi ya watu 5 waliouawa kinyama

T L