• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Haaland kuagana na Dortmund mwisho wa msimu huu wa 2021-22

Haaland kuagana na Dortmund mwisho wa msimu huu wa 2021-22

Na MASHIRIKA

WAKALA Mino Raiola amefichua kuwa kuna uwezekano mkubwa kwamba mteja wake Erling Braut Haaland ataagana na Borussia Dortmund ya Ujerumani mwishoni mwa msimu huu.

Japo kandarasi kati ya Dortmund na Haaland inatamatika 2024, ina kipengele kinachoruhusu kikosi kingine kuwania huduma zake kuanzia 2022 kwa ada ya Sh10.6 bilioni. Akiwa miongoni mwa masogora matata zaidi katika soka ya bara Ulaya, Haaland amefungia Dortmund mabao 51 kutokana na mechi 51 zilizopita za Bundesliga.

“Sote tulijua kwamba vikosi vingine vingewania huduma zake baada ya kujiunga na Dortmund. Huenda akaondoka muhula huu au huo utakaofuata. Lakini kuna uwezekano mkubwa kwamba hatua hiyo itafanyika mwisho wa msimu huu,” akasema Raiola.

Kwa mujibu wa Raiola anayewakilisha masupastaa wengi akiwemo kiungo Paul Pogba wa Manchester United, baadhi ya klabu zinazohemea Haaland ni Bayern Munich, Real Madrid, Barcelona, Chelsea na Manchester City. Haaland ambaye ni raia wa Norway, amefungia Dortmund mabao 74 kutokana na mechi 72 zilizopita katika mashindano yote tangu ajiunge nao kutoka Red Bull Salzburg ya Austria kwa Sh2.7 bilioni mnamo Disemba 2019. Alifungia Salzburg mabao 29 kutokana na mechi 27.

You can share this post!

Korir na Cheptonui kuongoza Wakenya 12 Malaga Marathon

Martial ataka aachiliwe na Man-United atafute hifadhi mpya...

T L