• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:25 PM
Dortmund wadengua Sevilla na kutinga robo-fainali za UEFA huku Haaland akivunja rekodi nne za ufungaji wa mabao katika UEFA

Dortmund wadengua Sevilla na kutinga robo-fainali za UEFA huku Haaland akivunja rekodi nne za ufungaji wa mabao katika UEFA

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Erling Braut Haaland, 20, alifungia klabu yake mabao yote mawili katika sare ya 2-2 iliyosajiliwa na waajiri wake Borussia Dortmund dhidi ya Sevilla ya Uhispania kwenye mchuano wa mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku.

Sare hiyo iliwezesha Dortmund ya Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kufuzu kwa robo-fainali za UEFA msimu huu baada ya kudengua Sevilla ya kocha Julen Lopetegui kwa jumla ya magoli 5-4.

Mabao yalifungwa na Haaland dhidi ya Sevilla yalifikisha idadi ya magoli yake kuwa 20 kutokana na mechi 14 zilizopita za kampeni za UEFA.

Haaland ambaye ni raia wa Norway, alifungulia Dortmund ukurasa wa mabao katika dakika ya 35 baada ya ushirikiano wake na nahodha Marco Reus kumwacha hoi kipa Yassine Bounou.

Bao la pili lililofungwa na Dortmund lilitokana na penalti iliyosababishwa na beki Jules Kounde aliyemchezea Haaland visivyo katika dakika ya 54.

Licha ya kufungwa mabao hayo mawili ya haraka, Sevilla walisalia imara na wakaendeleza mashabulizi dhidi ya wenyeji wao. Walipata penalti iliyofungwa na Youssef En-Nesyri katika dakika ya 68 kabla ya fowadi huyo raia wa Morocco kusawazisha mambo mwishoni mwa kipindi cha pili.

Dortmund kwa sasa wametinga robo-fainali za UEFA kwa mara ya kwanza tangu 2016-17 na watafahamu wapinzani wao katika hatua hiyo ya nane-bora baada ya droo ambayo imeratibiwa kufanyika Machi 19, 2021.

Haaland alifunga mabao mawili dhidi ya Sevilla siku tatu pekee baada ya kufunga magoli mengine mawili dhidi ya Bayern Munich kwenye Bundesliga. Hata hivyo, alipata jeraha lililomlazimu kuondoka uwanjani Allianz Arena katika kipindi cha pili cha mchuano huo ulioshuhudia Bayern ikisajili ushindi wa 4-2.

Haaland kwa sasa amefunga mabao mawili katika kila mojawapo ya mechi nne zilizopita za UEFA, ufanisi unaomfanya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufanya hivyo katika historia ya mapambano hayo ya bara Ulaya.

Hakuna mchezaji yeyote mwingine ambaye amefunga idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye UEFA kuliko Haaland tangu sogora huyo awajibishwe kwa mara ya kwanza kwenye kipute hicho mnamo Septemba 2019. Kigogo Robert Lewandowski wa Bayern amefunga magoli 19 pekee tangu wakati huo.

Akijivunia sasa magoli 20, Haaland ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufunga idadi hiyo ya magoli kwenye UEFA kabla ya kutimu umri wa miaka 21.

Rekodi hiyo ilikuwa awali ikishikiliwa na fowadi chipukizi wa Paris Saint-Germain (PSG), Kylian Mbappe aliyefunga magoli mabao 19 kwenye UEFA kabla ya kufikisha umri wa miaka 21.

Aidha, Haaland anakuwa mchezaji wa kwanza kuwahi kufikisha magoli 20 kwenye UEFA chini ya kipindi kifupi zaidi. Mshikilizi wa zamani wa rekodi hiyo, Harry Kane wa Tottenham Hotspur, alihitaji jumla ya mechi 24 kufunga mabao 20 katika soka ya UEFA.

Haaland pia amevunja rekodi ya kocha wa sasa wa Manchester United ambaye hadi Jumanne ya Machi 9, 2021, ndiye alikuwa mwanasoka raia wa Norway anayejivunia idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye soka ya UEFA.

Haaland kwa sasa anajivunia kufungia Dortmund jumla ya mabao 32 kutokana na mechi 30 za hadi kufikia sasa katika mashindano yote ya muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mashabiki wa Liverpool hawanitaki, wanataka Klopp asalie...

JAMVI: Kipute kikali kati ya Rais Kenyatta na Ruto...