• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Mechi bila starehe katika Kombe la Dunia

Mechi bila starehe katika Kombe la Dunia

CHRIS ADUNGO NA MASHIRIKA

MECHI za Kombe la Dunia, maarufu kama FIFA World Cup – mojawapo ya mashindano ya michezo yanayovumishwa zaidi duniani – zinaanza leo Jumapili nchini Qatar.

Na tofauti na makala mengine 21 ya awali ya Kombe la Dunia, fainali za kipute hicho nchini Qatar mwaka huu zitadhibitiwa na masharti makali zaidi.

Ni mara ya kwanza kwa michuano ya Kombe la Dunia kufanyika katika nchi ya Kiislamu, na imani ya kidini pamoja na misimamo mikali ya kitamaduni, imegeuka kuwa changamoto kubwa kwa waandalizi na mashabiki wa mapambano hayo makubwa zaidi ya kabumbu ulimwenguni.

Kinyang’anyiro hicho ambacho kinaanza leo Jumapili kitaendelea kwa siku 28 hadi Desemba 18. Timu 32 a kitaifa zitashiriki kwenye mechi 64 ambazo zinatarajiwa kuibua msisimko mkubwa.

Uuzaji wa pombe umedhibitiwa vikali, jambo ambalo limeibua hisia mseto miongoni mwa wadau na mashabiki wa mataifa 32 yanayoshiriki kivumbi hicho kinachodhaminiwa na kampuni kubwa ya bia, AB InBev, iliyo na makao makuu jijini Leuven, Ubelgiji.

“Kinyume na maagano ya awali, haitawezekana kwa yeyote kununua bia au vileo nje ya malango ya viwanja vyote vinane ambapo mechi zitaandaliwa,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa), Ijumaa.

Mashirika mbalimbali wafadhili wa mashindano hayo yamelalamikia kile yametaja kuwa ukiukaji wa mikataba kwenye mashindano hayo ya Kombe la Dunia.

Shirika la Kusimamia Kandanda Duniani (FIFA) linajikuna kichwa saa chache baada ya kulazimika kuharamisha matumizi ya pombe viwanjani kufuatia amri kutoka kwa serikali ya Qatar. Hatua hiyo imezua mkanganyiko mkubwa kuhusu kandarasi ya Dola 75M (Sh 9B) ambayo Fifa ilitia saini na Budweiser, Anheuser-Busch InBev.

Mwakilishi mwingine wa kampuni ya pombe ambaye hakutaka kutambuliwa alisema, washirika wengi ‘wamevunjwa moyo na Fifa kwa namna tofauti”.

Awali, mashabiki walio na tiketi za kuhudhuria michuano walikuwa na idhini ya kununua bia wakati wa mechi, katika muda wa saa tatu kabla ya mchuano na saa moja baada ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mechi kupulizwa.

Kampuni ya Budweiser imekashifu hatua ya utawala wa Qatar kutoruhusu uuzaji wa bia katika maeneo ya mashabiki wakati wa fainali za mwaka huu.

Ingawa pombe haijapigwa marufuku kabisa nchini Qatar, unywaji wake katika maeneo ya umma hauruhusiwi. Wasafiri hawawezi pia kuingia nchini humo wakiwa wamebeba pombe, hata kama wameinunua katika maduka yanayoiuza katika viwanja vya ndege vya taifa hilo.

Masharti mengine makali yanadhibiti aina ya mavazi, matumizi ya vyumba vya kulalia, usafiri wa umma na masuala ya uroda. Ni marufuku kwa mashabiki wa kike kuvalia nguo zinazoacha wazi sehemu kubwa ya miili yao katika taifa la Qatar ambako ushoga pia hauruhusiwi.

Aidha, wanawake na wanaume hawakubaliwi kubanana pamoja katika chombo kimoja cha kusafiria huku watakaotaka vyumba vya kulala kwa ajili ya kula uroda wakipata pigo. Kwa mujibu wa ripoti za vyanzo mbalimbali nchini Qatar, atatakiwa kuonyesha cheti cha ndoa ndipo aruhusiwe kulala chumba kimoja cha hoteli na mwanamke aliye naye.

Baadhi ya kanuni na itikadi kali za dini ya Kiislamu nchini Qatar zimelazimu wake na wachumba wa wanasoka wa Uingereza na Ujerumani kujihifadhia nafasi kwenye jahazi na meli maalumu zitakazotumiwa kwa ajili ya burudani kwenye forodha ya Doha.

Vipusa wa wachezaji wa timu ya taifa ya Uingereza walilazimika pia kusafiri hadi Qatar kwa ndege za kibinafsi ambazo zilikodishwa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA).

Zipo pia meli spesheli zitakazotumiwa na wachezaji wa Ujerumani kwa ajili ya huduma za ngono ya haraka baada ya kutoka katika hoteli zao za Souq Al-Wakra na Saoud bin Abdulrahman jijini Doha.

Kanuni hizo zimefanya taifa la Denmark kupiga marufuku wake na wachumba wa wachezaji wake kutua Qatar kwa kipindi kizima cha fainali za Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Denmark (DBU), maamuzi hayo ya kimakusudi yalichukuliwa ili “kuepuka migogoro na Qatar”.

You can share this post!

KIGODA CHA PWANI: Pwani waanza kutamauka kuhusu umoja wao...

JUNGU KUU: Mlima umeanza kumteleza Rais?

T L