• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
KIGODA CHA PWANI: Pwani waanza kutamauka kuhusu umoja wao kisiasa

KIGODA CHA PWANI: Pwani waanza kutamauka kuhusu umoja wao kisiasa

NA PHILIP MUYANGA

SUALA la umoja wa wanasiasa wa Pwani limekuwa likijadiliwa kwa muda mrefu, hususan kabla ya uchaguzi wowote mkuu ili wanasiasa, waweze kujipa uungwaji.

Wiki iliyopita Spika wa bunge la Seneti, Amason Kingi pamoja na mbuge wa Malindi Bi Amina Mnyazi, waliibua mchakato wa suala hilo la umoja wa wanasiasa wanaotokea eneo la Pwani, wakisema kuwa ni muhimu kwa maendeleo.

Lakini watu wengi wanajiuliza iwapo suala hilo limepitwa na wakati, kwani licha ya wanasiasa hao kulizungumzia, hawaoni suluhisho lolote au mwelekeo kuhusiana nalo.

Baadhi ya wakazi wa ukanda wa Pwani wanasema kuwa wanasiasa wamekuwa wakitumia suala hilo kwa manufaa yao ya kibinafsi. Wito huo huwa wa kuwaunganisha wanasiasa na si wananchi, ambao mara nyingi mahitaji yao hupuuzwa.

Hili wanasema kuwa, ni njia ambayo wanasiasa hutumia kupata kura kwa kulitaja suala la umoja. Endapo tu suala la umoja wa Pwani litajitokeza, mwanasiasa huwa anajitayarisha kwa uchaguzi.

Katika hafla moja ya mchango iliyofanyika kaunti ya Kilifi, Spika Kingi alizungumzia suala hilo. Alihoji kuwa iwapo wanasiasa wa ukanda wa Pwani hawataungana, hawataweza kuendeleza masuala muhimu katika bunge na hata kwenye meza ya uongozi wa kitaifa.

“Tusipoungana kisiasa tutafika Nairobi tukiwa vipande vipande, uzito wetu hautasikika ndani na nje ya bunge na kwenye meza ya kitaifa,” akasema Bw Kingi.

Huku akionekana kulenga siasa za mwaka wa 2027, Bw Kingi alisema kuwa ni vizuri Wapwani waweze kujiuliza, ni vipi kama ukanda utaweka mambo yake sawa na kuongea kwa usemi moja?

“Sisi tumejigawanyagawanya kama wanasiasa wa Pwani, ni mchanganyiko maalum,” akasema Bw Kingi, huku akihoji kuwa umoja wa wanasiasa wa eneo la Pwani, ndio nguzo ya kufaulisha maendeleo nchini.

Kulingana na baadhi ya wachanganuzi wa siasa, suala hilo la umoja wa Pwani hujadiliwa tu na wanasiasa kwa manufaa yao. Mara nyingi hawawahusishi wananchi katika mchakato huo mzima.

Wachanganuzi hao wanasema kuwa kumekuwa na mwito huo kwa miaka mingi kiasi cha kuwachosha wananchi kwa kuwa hakuna vitendo vyovyote wanaviona.

Kulingana na Bi Mnyazi, angependa kuona viongozi wa Pwani wameshikana kwa pamoja licha ya tofauti zao za kisiasa, ili kuwezesha kuendeleza Pwani.

“Tuweke kando tofauti zetu za kisiasa. Ni muhimu kusimama pamoja kwa manufaa ya watu wetu,” alisema Bi Mnyazi.

Kulingana na mchanganuzi wa siasa, Bi Maimuna Mwidau, suala la umoja wa wanasiasa wa Pwani limekuwako tangu jadi, kwa kuwa wanasiasa wameshindwa kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Uongozi sio tu kutoa wito.Ni lazima wananchi waone vitendo ili wafahamu kuna msukumo wa maendeleo,” anasema Bi Mwidau na kuongeza kuwa kiongozi yeyote anayetaja suala la umoja wa Pwani, lazima awe na nia ya kuunganisha wananchi pamoja.

Bi Mwidau anaeleza kuwa wananchi wanatafuta kiongozi anayewafaa, na suala la umoja wa Pwani linafaa kuambatana na vitendo vya viongozi wa ukanda wa Pwani.

Kwa upande wake mshauri wa masuala ya siasa Bw Bozo Jenje, wakati wa siasa umemalizika na ni sharti wananchi wa ukanda wa Pwani katika ngazi zote za kisiasa, kuwa kitu kimoja ili kutekeleza malengo ya wananchi.

“Umoja wa wanasiasa na wananchi wa Pwani utaweza kuleta maendeleo katika sekta mbalimbali kwa kuwa viongozi watakuwa na nguvu moja. Kwa hivyo wanaweza kubainisha shida za Wapwani kwa pamoja,” alisema Bw Jenje.

Aidha, mhadhiri wa masuala ya siasa wa chuo kikuu kimoja hapa nchini, ambaye alitaka jina lake libanwe, anasema kuwa suala la umoja wa wanasiasa wa Pwani haliwezi kufanikishwa. Kulingana naye hakuna kiongozi anayewashikilia Wapwani kama maeneo mengine.

“Ili umoja wa Wapwani upatikane, ni sharti kuwa na kiongozi mmoja kama vile marehemu Karisa Maitha na marehemu Shariff Nassir, ambao waliweza kusikika katika masula ya ukanda mzima wa Pwani,” asema mhadhiri huyo, akiongeza kuwa, kwa sasa suala hilo litabaki kuwa vivywani mwa wanasiasa tu kwani pia hao hawawahusishi wananchi katika kutafuta mwelekeo wa uongozi na umoja wa Wapwani.

“Itakuwa vigumu sana kwa wanasiasa kwa sasa kuwashawishi wananchi na kuwaambia kuna umuhimu wa kuwa na umoja wa wanasiasa wa Pwani, suala hilo limepitwa na wakati kwa sasa,” akasema mhadhiri huyo.

Ni muhimu pia iwapo wanansiasa watawaeleza wananchi umoja wanaouzungumzia ni wa nani. Je, ni umoja wa wanasiasa hao, ama ni umoja utakaolenga kuwahusisha Wapwani kuungana na kufanya maamuzi ya pamoja, kwa manufaa ya wakazi wa ukanda wa Pwani. Je umoja huo ni wa kisiasa pekee ama pia masuala mengine muhimu kama vile maendeleo ya kiuchumi, nafasi za kazi na kadhalika?

Kwa baadhi ya wakazi wa Pwani, ile siku wanasaisa wataungana na kuwa kitu kimoja na kutoa mwelekeo wa maendeleo ya ukanda wa Pwani, basi wananchi wanaweza kufaidi kimaendeleo.

  • Tags

You can share this post!

Mke wa Naibu Rais awahimiza wahubiri wajitokeze kukemea...

Mechi bila starehe katika Kombe la Dunia

T L