• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
JUNGU KUU: Mlima umeanza kumteleza Rais?

JUNGU KUU: Mlima umeanza kumteleza Rais?

NA WANDERI KAMAU

MASWALI yameibuka kuhusu iwapo Rais William Ruto ameanza kupoteza usemi wake katika ukanda wa Mlima Kenya, baada ya wabunge wa eneo hilo kumuasi kuhusu chaguo la watu watakaohudumu katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Kwenye mkutano wa wabunge ulioongozwa na Dkt Ruto mnamo Jumatano katika Ikulu, mrengo wa Kenya Kwanza uliidhinisha kuwaunga mkono Bw Hassan Omar, Bi Zipporah Kering, Bw Fred Muteti, Bw David Sankok na Bi Falhadha Dekow kuwania nyadhifa hizo.

Hata hivyo, duru zilieleza kuwa wabunge kutoka Mlima Kenya walihisi kutengwa, kwani hakukuwa na mtu hata mmoja kutoka ukanda huo.

Mwishoni mwa shughuli hiyo, wabunge hao walimpigia kura Bw Mwangi Maina, badala ya Bw Fred Muteti, aliyekuwa amependekezwa na Dkt Ruto.

Mbali na hayo, walimpigia kura aliyekuwa mbunge wa Kieni, Kanini Kega, licha ya kuwa katika mrengo wa Azimio la Umoja.

Naibu Rais Rigathi Gachagua asalimiana na mbunge maalum Sabina Chege majuzi PICHA | DPPS

Akihutubu katika eneo la Tharaka Nithi, Ijumaa, Naibu Rais Rigathi Gachagua alikiri kwamba ndiye aliyewarai wabunge kutoka ukanda huo kumuunga mkono Bw Kega, licha ya tofauti walizokuwa nazo kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Sisi tumetoka katika siasa. Hata jana mliona niliongea na hawa wabunge kutoka Mlima Kenya na kuwarai kumpigia kura Bw Kega licha ya kunitusi pamoja na Rais Ruto. Si walimpigia kura? Hatutaki kufuata mambo ya zamani. Lengo letu ni kuliunganisha eneo letu ili kuwa kitu kimoja na kuzungumza kwa sauti moja,” akasema Bw Gachagua.

Kutokana na hilo, wadadisi wa siasa wanasema mwelekeo huo unaashiria tofauti ambazo huenda zimeanza kujitokeza baina ya Rais Ruto na Bw Gachagua.

Wanasema ni kinaya kwa Bw Gachagua kuwarai wabunge wa Kenya Kwanza kumuunga Bw Kega mkono, ilhali mbunge huyo ni mshirika wa karibu wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Kilicho wazi katika mwelekeo huu ni kuwa kuna uwezekano mkubwa Rais Ruto akaanza kupoteza ushawishi wake katika Mlima Kenya, ikiwa wabunge wanaweza kumuasi na kumchagua mtu ambaye hakuwa amemwidhinisha,” asema Bw Oscar Plato, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Anasema hali hiyo inafaa kumtia hofu kuhusu mustakabali wa uhusiano baina yake na ukanda huo.

“Kauli ya Bw Gachagua kuwa eneo hilo linafaa kuungana inaonyesha ameanza kujijenga kisiasa. Hatua ya wabunge kuzingatia agizo lake inaonyesha ameanza safari ya kujikweza kisiasa kama kiongozi na msemaji wa kisiasa wa ukanda huo,” akasema Bw Plato.

Wadadisi wanasema si vigumu kwa Bw Kenyatta na Bw Gachagua kurejesha uhusiano wao, ikiwa Bw Gachagua amerejesha uhusiano wake na Bw Kega.

“Ikizingatiwa Bw Gachagua anaonekana kuanza kujijenga kisiasa kama kiongozi na msemaji wa Mlima Kenya, si vigumu kwake kurejesha uhusiano wake na Bw Kenyatta. Bw Gachagua ashawahi kuwa msaidizi wa kibinafsi wa Bw Kenyatta. Kama rais mstaafu, huenda Bw Kenyatta akaamua kumpa baraka Bw Gachagua kama mrithi wake kisiasa, kwani lengo kuu ni kuhakikisha maslahi ya kisiasa na kiuchumi ya ukanda huo yamezingatiwa,” asema mdadisi wa siasa Muchiri Kioi.

Katika hali hiyo, wanaonya Rais Ruto anafaa kutahadhari sana, kwani si vigumu kwa Bw Gachagua na Bw Kenyatta kuungana tena na kumzuia Dkt Ruto kupata uungwaji kwenye uchaguzi mkuu wa 2027.

“Ikimbukwe Bw Gachagua amekiri atafanya kila awezalo kuhakikisha maslahi ya Mlima Kenya yanazingatiwa kwa kila hali. Hayo ni masuala yanayopaswa kumfungua macho Rais Ruto kuhusu mustakabali wake wa kisiasa eneo hilo,” asema Bw Kioi.

You can share this post!

Mechi bila starehe katika Kombe la Dunia

MIKIMBIO YA SIASA: Mipasuko ya Mulembe ilivyomponza Kizito

T L