• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Mendy asimamishwa kazi na Man-City kwa hatia ya ubakaji

Mendy asimamishwa kazi na Man-City kwa hatia ya ubakaji

Na MASHIRIKA

BEKI Benjamin Mendy wa Manchester City ametiwa rumande baada ya kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka dhidi ya makosa manne ya ubakaji na hatia nyingine ya kumdhulumu mwanamke kimapenzi.

Nyota huyo raia wa Ufaransa mwenye umri wa miaka 27, anaripotiwa kutekeleza matendo hayo nyumbani kwake katika eneo la Cheshire, Uingereza kati ya Oktoba 2020 na Agosti 2021.

Kesi dhidi ya Mendy inahusisha wanawake watatu, mmoja kati yao akiwa na umri wa chini ya miaka 18.

Akiwa kizimbani katika mahakama ya Chester, Uingereza mnamo Agosti 27, Mendy alisalia kimya na maneno ya pekee aliyoyatamka ni kuthibitisha jina lake, anwani na tarehe ya kuzaliwa kwake.

Hata hivyo, hakuruhusiwa kujitetea kwa kuwa alipatikana na hatia nyingine ya kukiuka kanuni za dhamana mwanzoni mwa Agosti 2021.

Man-City tayari wamemsimamisha kazi beki huyo wa zamani wa AS Monaco. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wiki iliyopita, Mendy atasalia nje ya kikosi chao hadi uchunguzi dhidi yake utakapokamilika.

Mendy alitiwa nguvuni na maafisa wa usalama mnamo mnamo Agosti 26, 2021 akiwa katika kasri lake la Sh780 milioni katika mtaa wa Prestbury, eneo la Cheshire, Uingereza.

Mendy hudumishwa kwa mshahara wa Sh14 milioni kwa wiki ugani Etihad. Man-City walitumia kima cha Sh7.7 bilioni mnamo 2017 ili kumshawishi kuagana na AS Monaco ya Ufaransa na kujiunga nao.

Mechi yake ya mwisho kuchezea kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola ni ile iliyokamilika kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur katika ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu.

Mendy, 27, alikuwa sehemu ya wanasoka wa akiba Man-City walipokomoa Norwich City 5-0 katika EPL mnamo Agosti 21, 2021.

Licha ya kushuka kwa fomu yake na wingi wa visa vya majeraha kumweka nje ya michuano mingi ya Man-City tangu 2017, Mendy anajivunia tija ya kunyanyua mataji matatu ya EPL. Amechezea Man-City jumla ya mechi 50 pekee za EPL kufikia sasa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KASHESHE: Akanusha kuvaa vigodoro

Raila: Sehemu muhimu za chanjo ni sokoni, shuleni