• Nairobi
  • Last Updated May 30th, 2023 2:01 PM
Messi aagana na Barcelona kwa huzuni na machozi

Messi aagana na Barcelona kwa huzuni na machozi

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi, 34, amekiri kuna uwezekano mkubwa kwamba atajiunga na Paris Saint-Germain (PSG) japo kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) bado hakijaafikiana na mawakala wake.

Supastaa huyo raia wa Argentina alithibitisha hayo hapo jana alipokuwa akitoa hotuba rasmi ya kuagana na Barcelona ambao wamejivunia huduma zake kwa miaka 21 iliyopita.

Yalikuwa matamanio ya Messi kusalia ugani Camp Nou kusakatia Barcelona kwa mkataba mpya wa miaka mitano. Hata hivyo, kigezo cha jinsi ambavyo Barcelona wangemudu mshahara wake uliopunguzwa kwa asilimia 50, kilizima maazimio yake huku vinara wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) wakikosa kumsajili kwa ajili ya kampeni za msimu mpya wa 2021-22.

“Familia yangu pia ilikuwa na uhakika wa kuendelea kuishi hapa ‘nyumbani’ Catalonia. Lakini sasa huu ndio mwisho wa mahusiano na Barcelona na ni mwanzo wa maisha mapya kwingineko,” akasema Messi kwa kufichua kwamba huu ndio wakati mgumu zaidi anaoshuhudia kitaaluma.

“Nisingetaka kuagana na Barcelona – klabu ninayoipenda kwa dhati. Nilitamani kuondoka mwaka jana, si mwaka huu. Hiyo ndiyo sababu nina huzuni,” akaongeza huku akitiririkwa na machozi.

PSG walianza kuwasiliana na mawakala wa Messi mnamo Alhamisi iliyopita baada ya kudhihirika kwamba Barcelona hawana uwezo wa kumdumisha mwanasoka huyo kimshahara ugani Camp Nou.

Siku moja baadaye, rais Joan Laporta alishikilia kuwa kumdumisha Messi ugani Camp Nou kungeweka Barcelona katika hatari ya kuyumba kifedha kwa kipindi cha zaidi ya miaka 50.

Messi amekuwa mchezaji huru tangu Julai 1, 2021 baada ya mkataba wake kutamatika rasmi kambini mwa Barcelona. Nahodha huyo wa Argentina, ndiye mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Barcelona baada ya kufunga mabao 672 na kutwaa mataji 10 ya La Liga, manne ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na saba ya Copa del Rey.

Anajivunia pia rekodi ya kunyanyua tuzo ya Ballon d’Or mara sita. Hapo jana, kocha Ronald Koeman wa Barcelona alisema anamtakia Messi kila la heri katika taaluma yake ya usogora.

“Yasikitisha na bado sijaamini kwamba hutaweza tena kuchezea Barcelona,” akasema mkufunzi huyo raia wa Uholanzi.

Iwapo atayoyomea Ligue 1, PSG sasa itakuwa kikosi kinachojivunia wavamizi bora zaidi duniani ikizingatiwa kwamba tayari ina Kylian Mbappe na Neymar Jr aliyewahi kucheza pamoja na Messi kambini mwa Barcelona kati ya 2013 na 2017 kabla ya kuhamia PSG kwa kima cha Sh26 bilioni.

Kati ya wanasoka wengine wa PSG ambao ni marafiki wa karibu wa Messi ni Angel di Maria, Leandro Paredes na Marco Verrati.

Uhamisho wa Messi hadi PSG hautakiuka kanuni za usajili za Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) ikizingatiwa kwamba wanasoka wengi waliojiunga na PSG muhula huu wamefanya hivyo bila ada yoyote. Baadhi yao ni Achraf Hakimi, Sergio Ramos, Georginio Wijnaldum na Gianluigi Donnarumma.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Corona: Onyo kuhusiana na utoaji chanjo kwa halaiki

Leicester roho juu baada ya kubwaga Man-City kwenye...