• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Messi aahidi Argentina makuu Qatar

Messi aahidi Argentina makuu Qatar

NA MASHIRIKA

LIONEL Messi ametoa ahadi ya kuongoza Argentina kujituma maradufu katika makala ya 22 ya Kombe la Dunia mwaka huu 2022 na kutwaa ufalme.

Kombe la Dunia ndilo taji la pekee ambalo Messi hajawahi kunyanyua katika taaluma yake ya usogora.

Supastaa huyo wa Paris Saint-Germain (PSG) anatazamiwa kushirikiana vilivyo na masogora wengine watano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) – Emiliano Martinez, Christian Romero, Lisandro Martinez na Alexis Mac Allister – ili kutambisha Argentina walioko katika Kundi C pamoja na Saudi Arabia, Mexico na Poland.

Fainali za mwaka huu ni za tano kwa Messi na za mwisho kwa nyota huyo akivalia jezi za Argentina waliotawazwa wafalme wa dunia mnamo 1978 na 1986.

Argentina walinyanyua taji la Copa America kwa mara ya kwanza tangu 1993 mnamo Julai 2021 na wakafuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar bila kushindwa.

Chini ya kocha Lionel Scaloni, Argentina wanajivunia mseto wa chipukizi na wanasoka wazoefu kama vile Messi, 35 na Angel di Maria, 34 ambao watashirikiana vilivyo na Paulo Dybala, Julian Alvarez na Lautaro Martinez katika safu ya mbele.

Miamba hao walioambulia nafasi ya pili kwenye Kombe la Dunia mnamo 1990 na 2014, hawajapoteza mechi yoyote kati ya michuano 35 iliyopita.

Wataanza kampeni zao nchini Qatar dhidi ya Saudi Arabia mnamo Novemba 22 kabla ya kuvaana na Mexico kisha Poland mnamo Novemba 26 na 30 mtawalia.

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Tunisia roho juu kwamba watakuwa...

SHINA LA UHAI: Zijue faida za yoga kwa afya ya mwili kwa...

T L