• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mfalme wa soka Afrika

Mfalme wa soka Afrika

Na MASHIRIKA

RABAT, Morocco

SADIO Mane ameingia ligi ya wachezaji walioshinda tuzo ya mwanasoka bora (mwanamume) mara mbili barani Afrika.

Nahodha huyo wa Senegal alitunukiwa tuzo hiyo kwenye hafla ya kutangaza mshindi ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) mjini Rabat, Morocco, Alhamisi.

Mshambulizi huyo alikuwa Morocco kupokea zawadi yake, chini ya saa 24 baada ya kusakatia waajiri wake Bayern Munich kwa mara ya kwanza kabisa.

Bayern iko nchini Amerika kwa maandalizi ya msimu mpya.Kwa mwaka wa pili mfululizo wa tuzo hizo, Mane alibwaga Mohamed Salah wa Liverpool ambayo Mane alichezea kabla ya kujiunga na Bayern kwa Sh4.9 bilioni mwezi Juni.

Kipa wa Senegal na klabu ya Chelsea, Edouard Mendy alimaliza katika nafasi ya tatu.Mvamizi Salah kutoka Misri aling’ara kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu uliopita.

Alinyakua ‘kiatu cha dhahabu’ kwa kutinga mabao 23 na pia kusuka pasi nyingi zilizoishia nyavuni (13).

Hata hivyo, hiyo haikutosha kumnyima Mane tuzo hiyo ya kifahari kwa sababu, mara mbili, Mane alimzidia maarifa Salah katika ulingo wa kimataifa.

Mane aliongoza Senegal kushinda Kombe la Afrika kwa mara ya kwanza katika historia nchini Cameroon mwezi Februari.

Timu yake ya Teranga Lions iliilemea Misri kwa njia ya penalti (4-2) katika fainali ya Februari 8.Mwezi uliofuata, Teranga Lions pia waling’ata Mafirauni kwa njia ya penalti 3-1 na kuingia Kombe la Dunia litakalofanyika Novemba 21 hadi Desemba 18 nchini Qatar.

Mendy pia alichangia pakubwa katika mafanikio ya Senegal pamoja na kuisaidia Chelsea kutamba katika soka ya Klabu Bingwa Ulaya akiwa mchumani mwa The Blues mwezi Februari.

Mendy, 30, ni kipa wa kwanza kumaliza tuzo hizo ndani ya mduara wa tatu-bora katika kitengo cha mwanasoka bora wa Afrika tangu 2014 baada ya Vincent Enyeama kukamata nafasi ya tatu.

Mane sasa anaingia katika orodha ya wanasoka sita ambao wameibuka wanasoka bora mara mbili. Wengine ni Salah 2017 & 2018), Didier Drogba (2006 & 2009), Roger Milla (1976 & 1990), Nwankwo Kanu na El Hadji Diouf (2001 & 2002).

George Weah na Abedi Pele walinyakua tuzo hiyo mara tatu nao Samuel Eto’o na Yaya Toure mara nne.

Washindi wa tuzo za CAF 2022: Mwanasoka bora wa mwaka (mwanamume): Sadio Mane (Senegal & Bayern Munich); Mwanasoka bora wa mwaka (mwanamke) Asisat Oshoala (Nigeria & Barcelona); Kocha bora (mwanamume) Aliou Cisse (Senegal); Kocha bora (mwanamke) Desiree Ellis (Afrika Kusini); Timu ya taifa ya mwaka (wanaume) Senegal; Timu ya taifa ya mwaka (wanawake) itachaguliwa baada ya fainali ya Kombe la Afrika (Wafcon) kati ya Afrika Kusini na wenyeji Morocco leo Jumamosi; Chipukizi bora wa mwaka (mwanamke) Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas/Alvaldsnes); Chipukizi bora wa mwaka (mwanamume) Pape Matar Sarr (Senegal & Tottenham Hotspur); Klabu bora ya mwaka (wanawake) Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini); Klabu bora ya mwaka (wanaume); Wydad AC (Morocco); Mchezaji bora wa klabu za Afrika (mwanamke) Evelyn Badu (Ghana & Sekondi Hasaacas/Alvaldsnes); Mchezaji bora wa klabu za Afrika (mwanamume) Mohamed El Shenawy (Misri & Al Ahly); Bao kali la mwaka Pape Ousmane Sakho (Senegal & Simba).

You can share this post!

Wanawake na wasichana Kilifi hatarini kiafya kwa kukosa...

Naibu Rais apuuza umaarufu wa Raila maeneo ya Pwani

T L