• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 7:02 PM
Naibu Rais apuuza umaarufu wa Raila maeneo ya Pwani

Naibu Rais apuuza umaarufu wa Raila maeneo ya Pwani

NA JURGEN NAMBEKA

MGOMBEA wa urais wa chama cha UDA, Naibu Rais William Ruto na viongozi wengine wa muungano wa Kenya Kwanza, wamemsuta mgombea urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Bw Raila Odinga kwa kudai kuwa pwani ni ngome yake.

Hii ni licha ya kura ya maoni ya Infotrak kuonyesha kuwa Bw Odinga anaongoza kwa umaarufu katika kaunti zote sita za Pwani.

Wakizungumza wakati wa kampeni katika eneo la Old Town, jijini Mombasa, waliwataka wananchi wasimpigie kura Bw Odinga, wakidai kuwa ukakamavu aliokuwa nao wa kisiasa umekwisha.

“Bw Odinga tuliyemjua sasa amekwisha. Hawezi kusema ya kwamba ana ngome hapa Pwani. Tukiangalia vizuri, Naibu wa Rais ashapita katika maeneo yote na kubadilisha mambo. Kule Magharibi alishawachukua Bw Mudavadi na Bw Wetangula na sasa kura za huko zimegawanyika. Hapa Mombasa hali ni ile ile,” alisema gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua.

Gavana wa Kilifi Bw Amason Kingi alihoji kuwa Bw Odinga alikuwa amewasaliti Wapwani na hakustahili kupata kura za Wapwani.

“Yule mzee siku hizi amebadilika. Hapo zamani Bw Odinga alikuwa wa kwanza kuwatetea Wapwani. Yeye Raila Odinga amebadilika na amewasaliti wapwani. Tunataka kumwambia Bw Raila kuwa Pwani sio chumba chake cha kulala. Tutamwonyesha Agosti 9 kuwa, Dkt Ruto anaweza kumshinda,” alisema Gavana wa Kilifi, Amason Kingi.

Naibu wa Rais aliwaomba Wapwani wamuunge mkono kwani muda wa kuchaguliwa viongozi ulikuwa umekwisha.

Aliwataka wakazi wa jiji la Mombasa kumpa nafasi ili ainue maisha yao na kuwawezesha kiuchumi.

“Nataka tuunde serikali mpya ikifikia Agosti 9. Imesalia siku 16 na mna uwezo wa kutengeneza serikali ambayo inajali mtu wa chini. Si mmesema mna kura?” alisema Dkt Ruto.

Naibu wa rais alisisitiza kuwa atarejesha operesheni za bandari ya Mombasa na kuwapa mashamba maskwota iwapo atachaguliwa kuwa rais wa tano.

“Tulipojenga reli ya kuja hapa Mombasa maono yetu hayakuwa kutoa operesheni za bandari hapa. Tulitaka kutengeneza sehemu maalum ya viwanda ili vijana wapate kazi. Nikichaguliwa ninaahidi kuwa nitairejesha. Isitoshe, nimesikia kuwa Wapwani wanahangaika na suala la uskwota; hilo nitalishughulikia,” alisema Dkt Ruto.

Mgombea huyo wa urais ameeleza kuwa serikali yake itanunua ardhi kwa wamiliki wa ardhi ambao hawapo nchini kuwapa makazi Wapwani ambao wanateseka kwa kukosa makazi.

“Kama tulivyofanya kwa kununua ardhi ya kibinafsi na kuwapa makazi Wakenya, ndivyo nitafanya nikiingia serikalini. Tutanunua ekari milioni moja ili suala la Pwani tulimalize,” alisema Dkt Ruto.

Alimtaka Bw Odinga kutosumbua Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwani Wakenya walikuwa tayari kupiga kura.

Alidai kuwa pingamizi zote za Bw Odinga ni njama ya kuiba kura.

  • Tags

You can share this post!

Mfalme wa soka Afrika

Adai Joho amzuia kuonana na Raila

T L