• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Morans yaimarika kwenye viwango bora vya mpira wa vikapu duniani

Morans yaimarika kwenye viwango bora vya mpira wa vikapu duniani

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya wanaume ya Kenya ya mpira wa vikapu imepaa nafasi tatu kwenye viwango bora vya Shirikisho la Mpira wa vikapu duniani (FIBA) ambavyo vimetangazwa Machi 2, 2021.

Morans, jinsi timu hiyo inafahamika kwa jina la utani, imeruka kutoka 115 hadi 112 baada ya kuduwaza miamba Angola katika mojawapo ya mechi zake za Kundi B za kufuzu kushiriki Kombe la Bara Afrika (AfroBasket) jijini Yaounde, Cameroon.

Vijana hao wa kocha Elizabeth Mills, ambao walijikatia tiketi ya dimba hilo litakaloandaliwa nchini Rwanda baadaye mwaka huu, wamesukuma chini Suriname, Hong Kong na Congo Brazzaville nafasi moja kipa mmoja.

Washindi hao wa nishani ya fedha kwenye Kombe la AfroCan 2019 wanakamata nafasi ya 19 barani Afrika.

Morans walifuzu kurejea kwenye AfroBasket baada ya miaka 28 walipomaliza Kundi B katika nafasi tatu za kwanza. Walipoteza dhidi ya Senegal 69-51 (Februari 19) na Msumbiji 71-44 (Februari 21) na kulemea Angola 74-73 (Februari 20). Walikuwa wameandikisha ushindi dhidi ya Msumbiji 79-62 (Novemba 27) na kupoteza dhidi ya Senegal 92-54 (Novemba 25) na Angola 83-66 (Novemba 26) katika mechi za raundi ya kwanza za kundi hilo jijini Kigali, Rwanda.

Nigeria (nambari moja Afrika), Senegal (nne), Misri (sita), Morocco (nane), Jamhuri ya Afrika ya Kati (10) na Chad (18) ndizo timu pekee zilizokwamilia nafasi zao kwenye mduara wa 20-bora barani Afrika. Zinapatikana katika nafasi ya 22, 35, 60, 69 na 106 duniani, mtawalia.

Angola na Tunisia zimeteremka nafasi moja kila mmoja hadi 33 na 34 duniani nayo Ivory Coast inafunga tano-bora barani Afrika baada ya kutupwa chini nafasi mbili duniani hadi nambari 50.

Misri inaongoza kanda ya tano (Zone 5) ikifuatiwa na Rwanda (juu nafasi nne hadi 91 duniani), Sudan Kusini (imepaa kutoka 98 hadi 97 duniani), Uganda (imeshuka nafasi moja hadi 98 duniani), Kenya (imeimarika kutoka 115 hadi 112 duniani) nayo Burundi imepanda nafasi moja hadi nambari 125 duniani. Somalia, Tanzania na Eritrea zinasalia katika nafasi ya 144, 160 na 167 duniani, mtawalia.

Viwango bora vya Shirikisho la Mpira wa vikapu duniani vinavyohusisha mataifa 168, vinaongozwa na Amerika inayofuatwa na Uhispania, Australia, Argentina na Serbia katika usanjari huo.

  • Tags

You can share this post!

Wanahabari wataka waorodheshwe kwa watakaopewa chanjo ya...

Lengo ni kusalia kwa tano bora ligini – Mwatate FC