• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morocco kigezo wakifungua kampeni za Kundi F dhidi ya Croatia ugani Al Bayt

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Morocco kigezo wakifungua kampeni za Kundi F dhidi ya Croatia ugani Al Bayt

Na MASHIRIKA

MOROCCO na Croatia watafungua kampeni zao za Kundi F kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo Novemba 23, 2022.

Kukamilika kwa pambano hilo litakalopigiwa ugani Al Bayt kutapisha mchuano mwingine wa Kundi B kati ya Ubelgiji na Canada saa tisa baadaye.

Tangu mwanzo wa 2000, Morocco ambao ni miongoni mwa wawakilishi watano wa bara la Afrika nchini Qatar, hawakuwahi kunogesha makala manne ya Kombe la Dunia hadi mwaka wa 2018 nchini Urusi.

Japo walijizolea alama moja pekee nchini Urusi, walijituma vilivyo katika kampeni hizo walizozifungua kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Iran. Walipokezwa kichapo sawa na hicho walipokutana na Ureno kabla ya kufunga mechi za Kundi B kwa sare ya 2-2 dhidi ya Uhispania walionyanyua ubingwa wa 2010 nchini Afrika Kusini.

Tangu wadenguliwe mapema kwenye fainali za Kombe la Dunia 2018, Morocco waliaga fainali za Kombe la Afrika (AFCON) katika raundi ya 16-bora na robo-fainali mnamo 2019 na 2021 mtawalia.

Hata hivyo, wataanza kampeni za Kombe la Dunia mwaka huu wa 2022 wakijivunia rekodi nzuri ya kutopigwa katika mechi tano mfululizo. Walikomoa Chile (2-0) na Georgia (3-0) kabla ya kuambulia sare tasa dhidi ya Paraguay mnamo Septemba 2022.

Kikosi hicho kinachokamata nafasi ya 22 kimataifa, sasa kinanolewa na kocha Walid Regragui ambaye ana kibarua kizito cha kuongoza masogora wake kukahimili ushindani mkali wa Kundi F linalojumuisha pia Ubelgiji na Croatia waliopigwa na Ufaransa 4-2 kwenye fainali ya 2018 jijini Moscow, Urusi.

Regragui anatarajiwa kuunga kikosi thabiti kinachojivunia maarifa ya Sofyan Amrabat kwenye safu ya kati. Atashirikiana vilivyo na nahodha Romain Saiss, Achraf Hakimi, Nayef Aguerd ambao watapiga jeki wavamizi Youssef En-Nesyri na Hakim Ziyech.

Mshambuliaji wa Croatia Andrej Kramaric asherehekea baada ya kufunga bao wakicheza mechi ya kirafiki dhidi ya Saudi Arabia jijini Riyadh, Saudi Arabia mnamo Novemba 16, 2022. PICHA | AFP

Tegemeo kubwa la Croatia ni vigogo Luka Modric na Mateo Kovacic.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MKU yatoa chakula cha msaada na bidhaa nyingine muhimu Kitui

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Tunisia wasema wako tayari kwa...

T L