• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 9:50 AM
Morocco wakomoa Ghana katika gozi kali la Kundi C kwenye AFCON

Morocco wakomoa Ghana katika gozi kali la Kundi C kwenye AFCON

Na MASHIRIKA

BAO la dakika ya 82 kutoka kwa Sofiane Boufal lilisaidia Morocco kuvuna ushindi muhimu wa 1-0 dhidi ya Ghana katika gozi kali la Kundi C kwenye fainali za AFCON zinazoendelea nchini Cameroon.

Mvamizi huyo wa zamani wa Southampton ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) alichuma nafuu kutokana na utepetevu wa mabeki wa Ghana na kumwacha hoi kipa Jojo Wallocott katikati ya michuma ugani Ahmadou-Ahidjoe, Yaounde.

Morocco walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kuendeleza rekodi ya kushinda mechi zote sita za kufuzu kwa mchujo wa kuwinda tiketi za kushiriki fainali zijazo za Kombe la Dunia mnamo Disemba 2022 nchini Qatar.

Hata hivyo, mabingwa hao wa AFCON 1976 walitolewa jasho kabla ya kuzamisha Ghana ambao ni mabingwa mara nne wa taji la kipute hicho.

Beki mahiri wa Wolves ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Romain Saiss na kiungo Samy Mmaee walipoteza nafasi maridhawa za kuwaweka Morocco kifua mbele mwanzoni mwa kipindi cha kwanza.

Licha ya kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, Morocco ya kocha Vahid Halilhodzic nusura ijikute chini katika dakika ya 73 baada ya Joseph Paintsil kumvurumishia kipa Yassine Bounou kombora zito lililombabatiza.

Nahodha wa Ghana, Andre Ayew pia alimwajibisha vilivyo kipa Boufal wa Morocco ambaye sasa anasakata soka ya kulipwa kambini mwa Angers ya Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1).

Morocco almaarufu The Atlas Lions, sasa wanajiandaa kumenyana na Comoros mnamo Januari 14, 2022 kabla ya Ghana kushuka ulingoni kupimana ubabe na Gabon waliokuwa wenyeji wa AFCON mnamo 2017.

Black Stars ya Ghana ilishuka dimbani ikiwa na ari ya kuanza kampeni za kuwania taji la tano la AFCON kwa matao ya juu. Ushindi kwa Morocco sasa unawaweka pazuri kusonga mbele kutoka Kundi C na hatimaye kumaliza ukame wa miaka 45 tangu watawazwe wafalme wa bara Afrika mnamo 1976.

Morocco walifuzu kwa fainali za AFCON mwaka huu baada ya kudhibiti kilele cha Kundi E, na ni miongoni mwa timu nane zilizojikatia tiketi bila kupoteza mchuano wowote.

Walishinda mechi nne na kuambulia sare mara mbili na hivyo kujizolea alama 14, tano zaidi kuliko nambari mbili Mauritania ambao sasa wako katika Kundi F linalojumuisha pia Mali, limbukeni Gambia na mabingwa wa 2004, Tunisia.

Morocco walijibwaga ugani dhidi ya Ghana mwezi mmoja baada ya Algeria walioishia kutawazwa mabingwa wa Arab Cup mnamo Disemba 2021 kuwadengua kwenye robo-fainali za kivumbi hicho kwa penalti 5-3 baada ya sare ya 2-2 kufikia mwisho wa muda wa ziada.

Kabla ya kichapo hicho, Morocco walikuwa wameshinda mechi 19 na kupiga sare tatu kutokana na mechi 22 tangu wabanduliwe na Benin kwa penalti 4-1 baada ya sare ya 1-1 kwenye robo-fainali za AFCON 2019 nchini Misri.

Zaidi ya Misri (mataji saba) na Cameroon (mataji manne), Ghana ndicho kikosi cha tatu kinachojivunia mafanikio makubwa zaidi kwenye kipute cha AFCON baada ya kutwaa ubingwa mara nne – 1963, 1965, 1978 na 1982.

Hata hivyo, walishinda taji hilo mara ya mwisho miongo minne iliyopita walipozamisha wenyeji Libya kwa penalti 7-6 baada ya sare ya 1-1 kwenye fainali ya 1982. Ingawa wametinga fainali ya AFCON mara tatu tangu wakati huo, bahati imekuwa ikikosa kusimama nao, mara ya mwisho ikiwa 2015 walipozidiwa ujanja na Ivory Coast kwa penalti 9-8 baada ya sare tasa chini ya dakika 120 nchini Equatorial Guinea.

Masogora hao wa kocha Milovan Rajevac walifuzu kwa fainali za mwaka huu baada ya kushinda mechi nne, kupiga sare moja na kupoteza mechi moja. Walijizolea alama 13 na kudhibiti kilele cha Kundi C mbele ya Sudan ambao kwa sasa wako katika Kundi D pamoja na Guinea-Bissau, Misri na Nigeria ambao ni mabingwa mara tatu wa AFCON.

Ghana walijibwaga ulingoni dhidi ya Morocco wakilenga kujinyanya baada ya mabingwa watetezi Algeria kuwatandika 3-0 kwenye mchuano wa kirafiki uliowakutanisha nchini Qatar mnamo Jumatano iliyopita.

Morocco waliokosa huduma za Hakim Ziyech wa Chelsea, walitegemea zaidi maarifa ya Saiss (Wolves, Uingereza), Achraf Hakimi (PSG, Ufaransa), Abdessamad Ezzalzouli (Barcelona) pamoja na nyota Yassine Bounou, Munir El Haddadi na Youssef En-Nesyri wanaosakatia Sevilla ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Macho ya karibu kwa upande wa Ghana yalielekezwa karibu zaidi kwa nyota watatu wa EPL – Thomas Partey (Arsenal), Daniel Amartey (Leicester City) na Jordan Ayew (Crystal Palace) ila wakashindwa kuridhisha matamanio ya mashabiki wao.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

AFCON: Gabon wazamisha limbukeni Comoros katika Kundi C

Simiyu afurahishwa na matayarisho ya Shujaa

T L