• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
AFCON: Gabon wazamisha limbukeni Comoros katika Kundi C

AFCON: Gabon wazamisha limbukeni Comoros katika Kundi C

Na MASHIRIKA

BAO la kipindi cha kwanza kutoka kwa Aaron Boupendza lilitosha kuwavunia Gabon ushindi wa 1-0 dhidi ya limbukeni Comoros katika mchuano wa Kundi C kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Jumatatu usiku nchini Cameroon.

Fowadi Louis Ameka wa Gabon aliwazidi ujanja mabeki wa Comoros na kumwandalia Boupendza krosi safi katika dakika ya 16. Goli hilo lilichangia motisha ya Gabon waliovamia zaidi lango la Comoros na kumshughulisha vilivyo kipa Ali Ahamada kupitia kwa Denis Bouanga.

Comoros walizidiwa maarifa katika takriban kila idara na wakaachia Gabon waliokuwa wenyeji wa fainali za AFCON 2017 kutamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira.

Gabon kwa sasa wanajivunia alama tatu kileleni mwa Kundi C sawa na Morocco waliofungua kampeni zao za makundi kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Ghana ambao ni wafalme mara nne wa AFCON.

Comoros walifuzu kwa fainali za AFCON mwaka huu baada ya kuambulia nafasi ya pili nyuma ya Misri kwenye kipute cha kufuzu kutoka Kundi G lililojumuisha pia Kenya na Togo. Ingawa walianza mechi kwa matao ya juu huku wakimwajibisha vilivyo kipa Jean-Noel Amonome, makali yao yalishuka na pumzi zikaonekana kuwaishia baada ya Gabon wanaojivunia kutinga hatua ya robo-fainali za AFCON mara mbili kufunga bao.

Gabon walikuwa bila mshambuliaji na nahodha wao, Pierre-Emerick Aubameyang wa Arsenal ambaye alipatikana na virusi vya corona wikendi iliyopita.

Comoros kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Morocco mnamo Ijumaa ya Januari 14, 2022 kabla ya Gabon kushuka dimbani kupepetana na Ghana siku hiyo.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Madaktari 10 wa Mombasa kufaidika kwa mafunzo zaidi nchini...

Morocco wakomoa Ghana katika gozi kali la Kundi C kwenye...

T L