• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 2:49 PM
Simba SC yatangaza rasmi kutalikiana na Kahata, kiungo huyo sasa anamezewa mate na Al-Merrikh Sudan

Simba SC yatangaza rasmi kutalikiana na Kahata, kiungo huyo sasa anamezewa mate na Al-Merrikh Sudan

Na GEOFFREY ANENE

NI rasmi sasa kuwa Mkenya Francis Kahata si mchezaji wa Simba SC baada ya klabu hiyo kutangaza Jumamosi imeagana naye kwaheri.

Kupitia mitandao yao ya kijamii, miamba hao wa Tanzania wamemtakia kiungo huyo mema kwa kusema, “kila la kheri katika maisha yako mengine nje ya klabu yetu”.

Mabingwa hao wa Tanzania walisema kuwa siku zote watakumbuka utumishi wake “uliotukuka kwetu”. “Umeacha alama kubwa”.

Simba, ambao walisaini Kahata kutoka miamba wa Kenya, Gor Mahia mwaka 2019 kwa kandarasi ya miaka miwili, walimmiminia sifa.

“Ufundi wa miguu yako na mapenzi yako kwa Simba ni kielelezo cha uchezaji wenye moyo na kujitolea kwa klabu hii kubwa Afrika Mashariki,” walisema na kuamini “ipo siku unaweza kurudi hapa nyumbani tena.”

Kahata alijiriwa na Simba mnamo Julai 4, 2019 kwa mkataba wa unaoaminika kuwa Sh13 milioni.

Katika mpango huo, alifaa kupokea mshahara wa Sh350,000 kila mwezi, kupewa nyumba ya kuishi pamoja na ada ya uhamisho ya Sh4 milioni.

Kandarasi ya Kahata ilifaa kukatika rasmi Juni 30, 2021, lakini inaonekana wameelewana itamatishwe mapema. Ligi Kuu ya Tanzania ingali inaendelea.

Simba, ambayo pia imeajiri beki Mkenya Joash Onyango, inaongoza ligi hiyo ya klabu 18 kwa alama 67 baada ya kujibwaga uwanjani mara 27.

Ripoti za mwanzomwanzo baada ya tangazo la Simba na Kahata kuagana kwaheri zinasema kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 29 anamezewa mate na Al-Merrikh.

Akijiunga na miamba hao wa Sudan, atakuwa anachezea klabu yake ya nne ya kigeni. Alichezea timu ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini kati ya Julai na Desemba 2010 na KF Tirana kati ya Januari na Juni 2014 kwa mkopo kutoka Thika United. Miamba wa Albania, Tirana walimnyakua Januari 2015 kwa miezi sita kabla arejee nchini kuvalia jezi ya Gor na kisha kuelekea Simba.

You can share this post!

Mpango wa Tottenham kumwajiri kocha Antonio Conte watibuka

Wales na Albania waambulia sare tasa kwenye mechi ya...