• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Mtanange babkubwa

Mtanange babkubwa

LONDON, Uingereza

Na MASHIRIKA

MACHO yote leo yataelekezwa kwa washambuliaji Jamie Vardy na Pierre-Emerick Aubameyang wakati Leicester na Arsenal watavaana ugani King Power katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) inayopamba moto.

Mwingereza Vardy anajivunia kufungafunga Arsenal. Ametikisa nyavu za wanabunduki hao mara 11 ligini. Hakuna timu nyingine ya EPL ambayo amefunga mabao mengi kama hiyo.Aubameyang pia anapenda sana kucheka na nyavu za ‘mbweha’ hao.

Raia huyo wa Gabon amejaza wavuni mabao manne katika michuano saba iliyopita dhidi ya Leicester.Leicester ya kocha Brendan Rodgers ilipoteza mechi mbili zilizopita dhidi ya Arsenal ugani King Power kwa hivyo italenga kulipiza kisasi.

Ilizabwa 2-0 kupitia mabao ya Christian Fuchs (kujifunga) na Eddie Nketiah kwenye kipute cha Carabao mnamo Septemba 2020 kabla na kutupa uongozi ilipochapwa 3-1 ligini kupitia mabao ya David Luiz, Alexandre Lacazette na Nicolas Pepe.

Timu hizi zinakutana katika mashindano yote kwa mara ya 147. Vijana wa kocha Mikel Arteta wakitwaa ushindi leo watakuwa wameshinda Leicester mara tatu mfululizo tangu mwaka wa 1925. Leicester na Arsenal wanashikilia nafasi ya tisa na 10 mtawalia wakiwa wamezoa alama 14 kila mmoja.

Arsenal ilianza vibaya msimu kwa kupoteza michuano mitatu, lakini imedumisha rekodi ya kutoshindwa tangu Septemba 1 katika mashindano yote. Leicester haijapoteza michuano mitano iliyopita katika mashindano yote.

Mechi nyingine kubwa leo ni kati ya vijana wa kocha Ole Gunnar Solskjaer, Manchester United, na Tottenham ya kocha Nuno Espirito Santo. Wote wanauguza vichapo kutokana na mechi zao zilizopita. United iliabishwa 5-0 na Liverpool kupitia mabao ya Mohamed Salah (matatu), Naby Keita na Diogo Jota naye Michail Antonio akafungia West Ham bao lililozamisha Tottenham 1-0.

Solskjaer anakabiliwa na presha. “Mashetani wekundu” wameambulia alama moja pekee katika mechi nne zilizopita ligini baada ya kulemewa na Aston Villa 1-0, Leicester 4-2 na Liverpool na kutoka sare ya 1-1 dhidi ya Everton.

Wenyeji Tottenham wanashikilia nafasi ya sita kwa alama 15, moja nyuma ya nambari saba United. Wachana-nyavu matata Harry Kane (Tottenham) na Marcus Rashford (Manchester United) ni baadhi ya silaha zilizo na uwezo wa kuamua mwelekeo wa mechi hii.

United itakosa kiungo Paul Pogba aliyelishwa kadi nyekundu dhidi ya Liverpool. Macho pia yatakuwa kwa supastaa Cristiano Ronaldo. Viongozi wa sasa wa ligi Chelsea watalimana na wenyeji na mabwanyenye Newcastle wanaoshikilia nafasi ya 19 nao nambari mbili Liverpool wataalika Brighton inayoshikilia nafasi ya nne.

Mabingwa watetezi Manchester City, ambao ni nambari tatu, watamenyana na nambari 15 Crystal Palace ugani Etihad.

You can share this post!

Hatutaunga mwaniaji urais nje ya OKA- vinara

FC Barcelona katika mizani ya Alaves La Liga ikimsubiri Xavi

T L