• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Mwendwa aagizwa ajitenge na soka baada ya kuachiliwa

Mwendwa aagizwa ajitenge na soka baada ya kuachiliwa

RICHARD MUNGUTI na JOHN ASHIHUNDU

RAIS wa Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF), Nick Mwendwa amepata afueni baada ya kuachiliwa kwa dhamana ya Sh4 milioni pesa taslimu.

Akimwachilia kwa dhamana, hakimu mwandamizi Wandia Nyamu alimwamuru Mwendwa asiende karibu na afisi za afisi za FKF zilizoko Kandanda House, Kasarani.

Pia aliamriwa asihutubie wanahabari wala kuzungumza na wafanyakazi wa FKF. Mwendwa aliachiliwa baada ya kukaa seli siku tatu akihojiwa kuhusu ubadhirifu wa Sh38 milioni za FKF.

Mawakili Erick Mutua, Tom Ojienda, John Khaminwa, Nelson Havi, Mutula Kilonzo Junior na Sylvia Matasi waliambia mahakama kwamba polisi walipotosha umma walipodai Mwendwa amefuja Sh513 milioni za FKF.

Mutua aliambia hakimu polisi na maafisa wakuu Serikali walipotosha umma kwa madai hayo yasiyo na msingi.

Mahakama iliambiwa masuala ya kandanda nchini hayahusiani na utenda kazi wa Serika kwa vile yanasimamiwa na mashirika ya Chama cha Soka barani Afrika (CAF) na Shirikisho la Kimataifa la Soka (Fifa).

Mutua aliwasisilisha Kortini barua kutoka kwa Fifa ya Novemba 14 ikitisha kuipiga marufuku Kenya kushiriki katika mechi za kimatifa iwapo Serikali haitakoma kuingilia masuala ya soka nchini.

“Kamati ya Ringera haitambuliwi na Fifa, na hata hawawezi kutekeleza majukumu ya FKF chini ya Mwendwa,” alisema Khaminwa.

Khaminwa aliongeza masuala ya kandanda yanasimamiwa na watu binafsi kama Mwendwa na wala sio Serikali.

Ojienda aliambia Korti kwamba iwapo Seriklai itaendelea kuvuruga utaratibu wa FKF, vilabu na wachezaji wa kandanda watateseka kwa kiasi kikubwa na wafanyakazi wa FKF hawatapata mishahara na marupurupu yao kwa vile Fifa na mashirika mengine yatakoma kufadhili shughuli za kandanda.

Haya yanajiri huku washikaji dau wa tabaka mbalimbali wakiendelea kumpongeza Waziri wa Michezo Amina Mohamed kufuatia hatua yake ya kuivunjilia mbali kamati ya Soka na kuteua kamati mpya ya muda kusimamia shughuli za mchezo huo nchini.

Timu za AFC Leopards, Gor Mahia Posta Rangers na Chama cha Wakufunzi wa Soka Nchini (Kefoca) zimesema Amina alichukua hatua nzuri kuondoka kamati ya Mwendwa na kuweka kamati mpya ya kushikilia usukani kwa muda wa miezi sita.

Amina aliivunjilia mbali kamati ya FKF Alhamisi iliyopita baada ya shirikisho hilo kufanyiwa uchunguzi wa kina kutokana na madai ya lilishindwa kueleza jinsi lilivyotumia Sh513 milioni zilizotengewa shughuli za kandanda nchini.

Katika taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari leo Jumatatu, mwenyekiti wa AFC Leopards Dan Shikanda alisema uamuzi wa waziri unalenga kuimarisha usimamizi wa mchezo huo kwa jumla.

“AFC Leopards ingependa kumshukuru Waziri Amina Mohamed pamoja na kamati iliyoteuliwa chini ya Jaji Mstaafu Aaron Ringera,” taarifa ya Ingwe iliongeza.

Sikanda alisema hatua hiyo itasaidia Wakenya kujipanga na kupigia watu wazuri wanaofaa kuongoza mchezo huo kuanzia mashinani.

Posta Rangers kupitia kwa mwenyekiti wao John Tonui ilisema: “Usimamizi wa Rangers utashirikiana kikamilifu na kamati ya muda katika kila jambo kwa lengo la kuhakikisha soka inasimamiwa ipasavyo.

Kenfoca Serikali ilitakiwa kuchukuwa hatua hiyo mapema zaidi ili Wakenya wapate watu wanaofaa katika uongozi wa soka nchini.

“FKF imekuwa ikijiingiza katika siasa za ubaguzi, huku watu wasiofaa wakipewa vyetu vya kuonyesha wamehitimu kama wakufunzi wa kandanda,” aliongeza kiongozi wa chama hicho Bob Oyugi.

Alisema kufanya vibaya kwa timu za Kenya katika mashindano ya kimataifa unatokana na uongozi duni wa afisi ya Mwendwa ambayo haina miundo misingi inayofaa

You can share this post!

Ann Kananu aapishwa rasmi kuiongoza Nairobi

Hatimaye Stars, Firat waonja ushindi

T L