• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Mwendwa akosa kufika kortini tena

Mwendwa akosa kufika kortini tena

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa hakufika katika mahakama ya Kiambu kujibu mashtaka mapya.

Hakimu mwandamizi K Sambu aliamuru tena Mwendwa afike kortini Julai 15, 2022 kushtakiwa.

Mnamo Julai 7, 2022, Sambu aliamuru Mwendwa ajisalamishe kortini kujibu shtaka kufuatia ombi la naibu mkurugenzi wa mashtaka ya umma (ADPP) Joseph Gitonga.

“Tuko na ushahidi mpya dhidi ya Mwendwa. Naomba hii mahakama iamuru Mwendwa afike kortini Julai 11,2022 kujibu mashtaka,” Gitonga alimraia Sambu.

Gitonga aliomba mahakama iamuru afisa anayechunguza kesi dhidi ya Mwendwa amkabidhi samanzi ya kufika kortini.

Lakini kulikuwa na sikukuu ya Waislamu Julai 11, 2022 na mahakama hazikuwa zikihudumu.

Mnamo Julai 6, 2022 hakimu mkuu Eunice Nyuttu alimwachilia Mwendwa baada ya kiongozi wa mashtaka kusema hakuwa na ushahidi katika kesi ya ufisadi wa Sh38 milioni dhidi ya kinara huyo wa zamani wa shirikisho la soka nchini.

Nyuttu alimwachilia Mwendwa chini ya kifungu nambari 87(a) cha sheria za uhalifu (CPC).

Chini ya kifungu hiki cha sheria, mmoja akiachiliwa anaweza akatiwa mbaroni na kushtakiwa upya.

Nyuttu alielezwa Waziri wa Spoti Amina Mohammed na wakuu wa benki ya KCB walikataa kuandikisha ushahidi wa ufujaji wa pesa za FKF na Mwendwa.

Kamati ya FKF ilitimuliwa Novemba 2021 na Mohammed akateua kamati chini ya uongozi wa Jaji (mstaafu) Aaron Ringera kusimamia masuala ya soka nchini.

Hatua ya kutimua FKF ilikuwa kiini cha Kenya kupigwa marufuku kushiriki katika mechi za Shirikisho la Soka Duniani-FIFA.

Mawakili Eric Mutua na Charles Njenga wamewasilisha kesi mahakama kuu kupinga Mwendwa akishtakiwa upya wakidai mwanachama mmoja wa kamati ya Jaji Ringera Hassan Haji ni nduguye Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Wanadai DPP alikuwa na sababu ya kushtaki Mwendwa kwa vile yuko na manufaa anayotaka katika kesi.

You can share this post!

Sakaja aruka kiunzi cha mwisho

Jubilee yasutwa kwa rekodi mbaya ya utetezi wa haki

T L