• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Mwendwa kushtakiwa upya mahakamani leo Jumanne

Mwendwa kushtakiwa upya mahakamani leo Jumanne

NA RICHARD MUNGUTI

ALIYEKUWA Rais wa Shirikisho la Soka Nchini (FKF) Nick Mwendwa atafika katika mahakama ya Kiambu leo Jumanne kujibu mashtaka mapya ya ufisadi wa Sh38 milioni.

Mwendwa aliyeachiliwa wiki iliyopita na hakimu mkuu mahakama ya kuamua kesi za ufisadi Eunice Nyuttu alipewa samanzi afike kortini leo Jumanne.

Nyuttu alimwachilia Mwendwa katika kesi iliyomkabili ya kuifuja FKF zaidi ya Sh38 milioni.

Bi Nyuttu alimwachilia Mwendwa alipoelezwa na Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) “ hakuna ushahidi dhidi ya Mwendwa.”

Hakimu aliombwa aahirishe kesi dhidi ya Mwendwa hadi Oktoba 2022 ushahidi kamili uwasilishwe kortini.

Lakini mawakili Eric Mutua na Charles Njenga walipinga ombi la DPP la kuahirisha kesi hadi Oktoba na kuomba korti imwachilie huru Mwendwa kwa vile miezi minane imepita na hakuna dalili ya ushahidi kuwasilishwa.

DPP aliomba Nyuttu amwachilie Mwendwa chini ya kifungu cha Sheria nambari 87(a) cha uhalifu.

Bi Nyuttu alimwachilia Mwendwa kisha akamweleza “atakamatwa na kufikishwa kortini siku ile ushahidi utakapopatikana kuendelea na kesi.”

Mnamo Julai 8,2022, naibu wa DPP Joseph Gitonga aliwasilisha ombi katika Mahakama ya Kiambu , Mwendwa ashtakiwe upya katika Mahakama ya Kiambu.

“Ni ukweli samanzi zilitolewa na mahakama ya Kiambu Mwendwa ajisalamishe kortini Julai 11,2022 kujibu mashtaka upya,” kiongozi wa Mashtaka Kaunti ya Kiambu Everlyne Onunga aliambia Taifa Spoti wakati wa mahojiano kwa njia ya simu.

Bi Onunga aliambia Taifa Spoti kuwa kesi dhidi ya Mwendwa itaongozwa na kundi maalum la viongozi wa mashtaka kutoka afisi kuu ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji.

Bi Onunga aliyekuwa akiongoza kesi hiyo dhidi ya Mwendwa kabla ya kuhamishwa kutoka Nairobi hadi Kiambu aliambia Taifa Spoti , kesi hiyo inayomkabili Mwendwa itaongozwa na maafisa kutoka afisi ya DPP, Nairobi.

Akiwasilisha ombi Mwendwa afikishwe kortini leo Jumanne, Gitonga aliambia korti “ushahidi mpya umepatikana dhidi ya Mwendwa. Atahitajika kujibu mashtaka upya.Kesi itaendelea hadi tamati.”

Hakimu mwandamizi K Sambu aliamuru Mwendwa afike kortini leo Jumanne kujibu shtaka.

  • Tags

You can share this post!

Chakula: Magoha awapa matumaini walimu wakuu

Raila kuzuru Pwani telezi

T L