• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 8:55 AM
Raila kuzuru Pwani telezi

Raila kuzuru Pwani telezi

LUCY MKANYIKA NA WINNIE ATIENO

MWANIAJI wa urais wa chama cha Azimio la Umoja-One Kenya, Bw Raila Odinga anaanza rasmi ziara ya eneo la Pwani huku mgawanyiko mkubwa ukiendelea kutishia kura zake.

Bw Odinga anatarajiwa Pwani leo Jumanne huku mshindani wake mkuu Dkt William Ruto (UDA) akinyemelea na kupata ufuasi katika eneo ambalo limekuwa ngome yake kwa miaka mingi.

Kesho Jumatano, Bw Odinga atakuwa katika Kaunti ya Kwale kujitafutia yeye pamoja na wawaniaji wa chama cha ODM uungwaji. Alhamisi atakuwa Mombasa na Ijumaa Kaunti ya Kilifi.

Katika Kaunti ya Taita Taveta, wawaniaji wa viti mbalimbali vya kisiasa wanaohusishwa na muungano wake, wametishia kutohudhiria mkutano wake wa leo.

Wanasiasa hao kutoka vyama vya ODM, Narc, Wiper, DAP-K na KANU, wamemlaumu Gavana Granton Samboja kwa kuugeuza mkutano wa Bw Odinga katika kaunti hiyo kuwa hafla yake.

Vita vya ubabe kati ya Bw Samboja na wagombeaji wengine kutoka vyama tanzu vya muungano wa Azimio, vimeonekana kuharibu kampeni za Bw Odinga.

Bw Raila ataanza ziara ya siku nne katika eneo la Pwani, kusaka uungwaji mkono katika uchaguzi mkuu ujao.

Katika kikao na wanahabari, wanasiasa hao walilalamikia kupuuzwa. Walieleza kuwa maoni yao ya kumtaka Bw Odinga kufanya mikutano yake katika maeneo ya Wundanyi, Mwatate na Voi yalikataliwa.

Viongozi hao walihoji kuwa, walifanya mkutano Julai 9 wa kujadili ziara ya Bw Odinga kwa sababu mkutano uliofanywa awali kupanga ziara hiyo, uliwahusisha tu wanachama wa vyama vya Jubilee na ODM pekee.

“Mkutano ulifanywa na sehemu za kufanya mikutano zikaamuliwa. Ila sehemu hizo hazifai kwa mgombeaji wa hadhi ya juu kama Bw Odinga. Kwa hivyo, maamuzi yaliyofanywa katika mkutano huo tumeyapuuzilia mbali,” alieleza Bi Patience Nyange wa Narc.

Aliongeza kuwa, iwapo malalamishi yao hayatasikilizwa, hawatakuwa na budi ila kususia mkutano wao na kisha kumwalika Bw Odinga wakati mwingine.

Haya yanajiri huku upinzani mkali ukiibuka katika kaunti hiyo, dhidi ya mpango wa kuwateua wagombeaji wenye umaarufu kuwania viti vya kisiasa ili kuisaidia Azimio kupata wajumbe wengi.

Katibu mkuu wa chama cha Wiper katika Kaunti ya Taita Taveta, Bw Peter Shambi katika kikao kingine na wanahabari, alieleza kuwa mkutano uliokuwa na wajumbe wa vyama vyote vya Azimio, waliafikiana kuwa Bw Odinga angefanya mkutano wake katika uwanja wa Dawson Mwanyumba saa nne asubuhi, kituo cha magari cha Mwatate saa saba, na uwanja wa mpira wa Tausa katika kaunti ndogo ya Voi saa tisa jioni.

“Tushawaambia wafuasi wetu wawe tayari kumkaribisha mpeperushaji bendera wetu. Waje kwa wingi. Kuna wale wanapanga kuuharibia sifa mrengo wetu ila tunaomba tudumishe amani wakati huu wa uchaguzi,” alisema.

Bw Shambi alieleza kuwa, tofauti zinazojitokeza huenda zikaathiri ngome za Bw Odinga licha ya uungwaji mkono kuwepo kutoka kwa mirengo hiyo yote.

Kulingana na mabango ya matangazo yanayosambazwa na kikosi cha kampeni za Bw Samboja, Bw Odinga atazuru Wasinyi (Wundanyi), Kilulunyi (Mwatate) na Mwakiki (Voi).

Katibu wa kitaifa wa maandalizi ya chama cha ODM kwa niaba ya Muungano wa Wanademokrasia Wanawake, Bi Hope Mwakio, ubaguzi wa wagombeaji wengine katika muungano huo hautakubaliwa.

“Wanataka tukubaliane na kumbi walizochagua lakini hatutakubaliana nao. Nilikuwa katika mkutano, kumbi hizo zilipokataliwa. Mpango wao sio wa kutafutia Bw Odinga kura,” alisema Bi Mwakio.

Alidai kuwa mipango iliyopendekezwa ni ya kumwaibisha Bw Odinga kwa kumfanya kukosa hadhira kubwa ipasavyo.

“Wanataka kupeleka mikutano katika kumbi walizochagua ili wajitafutie kura na kuongeza umaarufu wao. Cha muhimu ni Bw Odinga apate kura nyingi,” alisema Bi Mwakio.

Walieleza kuwa, tayari walikuwa washatuma malalamishi yao kwa Bw Odinga wakisubiri kumbi hizo zibadilishwe.

Katika kaunti ya Mombasa, na Kwale wakuu wa chama wamewasihi wagombea kujitayarisha kumkaribisha Bw Odinga.

  • Tags

You can share this post!

Mwendwa kushtakiwa upya mahakamani leo Jumanne

TAHARIRI: Ushuru wa ziada utumike kuokoa raia wa tabaka la...

T L