• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 1:14 PM
Ni wakati wa Harambee Starlets kung’aa – Beki

Ni wakati wa Harambee Starlets kung’aa – Beki

NA AREGE RUTH

BEKI wa kushoto wa Harambee Starlets Enez Mango anasema huu ndio wakati wa timu hiyo ya taifa kuonyesha ubabe kimataifa warembo wanapojipanga kupimana nguvu na Albania mwezi Aprili.

 Mchezaji huyo wa  timu ya Farul Constanta ya Ligi Kuu ya Wanawake nchini Romania, anakadiriwa kuwa mchezaji mwenye nidhamu zaidi kuwahi kuzalishwa na Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL).

Mango, Christine Awuor (Zetech Sparks), Lupemba Bilonda (Thika Queens) ni miongoni mwa mabeki sita ambao watakuwa wanajenga ukuta wa Starlets dhidi Albania.

Akizungumza na Taifa Spoti kwa njia ya simu, hakuficha furaha yake baada ya kutajwa kwenye kikosi cha Starlets.

“Ninashukuru pia kupata mwaliko, nitasafiri Jumapili kujiunga na wachezaji wenzangu kambini. Tumefurahi kurejea baada ya kuwa nje kwa muda wa mwaka mmoja,” alisema Mango.

“Ninafuraha kwamba, shirikisho halikuchukua muda mrefu kuandaa mchuano wa kirafiki wa wanawake. Hii inamaana kuwa, kuna mipango mingi ijayo ambayo itasaidia kukuza soka ya wanawake nchini,” aliongezea Mango.

Kwa upande wa mshambulizi wa Kisumu All Starlets Monica Etot, ambaye ambaye ni mfungaji bora wa pili KWPL na mabao 10 alipata mwaliko kwa mara ya kwanza.

“Sikutarajia kutajwa kwenye kikosi. Ni furaha ya kila mchezaji kuwakilisha taifa lake. Nitaendelea kufunga mabao nikipata nafasi ya kuwakilisha taifa langu,” alisema Etot.

Mshambulizi Mwanahalima Adams Jereko ambaye yupo kwenye kikosi ndiye mfungaji wa muda wote wa Starlets akiwa na mabao 16.

Monalizer Anyango (Zetech Sparks), Ketsi Ngaira (Ulinzi Starlets) na Valentine Khwaka (Gaspo Women) pia wameitwa Starlets kwa mara ya kwanza.

Wachezaji 16 wa ndani na 17 wanaochezea mataifa mengine wamejumuishwa katika Kikosi cha wachezaji 33 cha Starlets.

  • Tags

You can share this post!

Wanakuza Hass Avocado kuwafaa wakazi wa Gusii

Mwanamume kizimbani kwa kutishia kumuua mamake

T L