• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Nyanza Prisons yajiwekea malengo ya kunyakua taji la Afrika miaka mitano ijayo

Nyanza Prisons yajiwekea malengo ya kunyakua taji la Afrika miaka mitano ijayo

NA JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Maafande wa Nyanza Prisons ni kati ya vikosi ambavyo hushiriki kipute cha voliboli ya Ligi Kuu nchini.

Wanaume hao wanapatikana katika Magereza ya Kodiga, Kaunti ya Kisumu. Kipute cha msimu uliopita ndio ilikuwa mwanzo wa kikosi hiki kushiriki kampeni za Ligi Kuu.

”Ndio inaelekea kutinga miaka miwili tangia timu yetu ianzishwe lakini tuna ndoto ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu na kutwaa tiketi ya kushiriki kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CAVB) ndani ya miaka mitano ijayo,” alisema na kuongeza kuwa wanahitaji kushiriki mazoezi zaidi ili kujiweka vizuri maana wamegundua kampeni za kipute hicho hakuna mteremko.

”Baada ya kukamilisha msimu wa kwanza sasa tunawazia kampeni za muhula ujao ambazo zinazoratibiwa kuanza mwishoni mwa mwaka huu,” akasema na kuongeza kuwa wakali wa tangu jadi kwenye kipute hicho bado sio mchezo wanazidi kushusha ushindani wa kufa mtu.

Ingawa ndio mwanzo ilishiriki kipute hicho Nyanza Prisons ilijitahidi kiume na kumaliza ya kumi kwa kusajili alama 15 sawa na Administration Police Kenya (AP Kenya) tofauti ikiwa idadi ya seti za ushindi.

Kama kawaida wakali ngarambe hiyo na mabingwa watetezi Kenya

General Service Unit (GSU) ilimaliza kileleni kwa kuzoa alama 40 sawa na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA).

Wafalme wa zamani Kenya Prisons ilimaliza ya tatu kwa kukusanya alama 37, sawa na Trail Blazers tofauti ikiwa seti za ushindi.

Trail Blazers iliyoshiriki kipute kwa mara ya kwanza ilishangaza wapinzani wao kwa kuonyesha mchezo wa kuvutia na kuzuia Jeshi la Ulinzi (KDF) kutofuzu kushiriki fainali za mwaka huu.

Fainali za mwaka huu ambazo zimepangwa kuandaliwa katika ukumbi wa Karasani mwishoni mwa mwezi huu zitashirikisha: GSU, KPA, Kenya Prisons na Trail Blazers.

Ili kupaisha mchezo huo nchini anashikilia kuwa Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) linastahili kuandaa mashindano mengi ya timu za humu nchini pia za kimataifa.

”Pia KVF inapaswa kuhakikisha waamuzi pia makocha wa voliboli wamepokea mafunzo na kuhitimu kwa taalumu zao ili kusaidia katika makuzi ya mchezo huo,” akasema.

Naibu kocha, Oscar Wandera anasema kuendesha timu ya michezo bila fedha sio kibarua rahisi.

Anatoa wito kwa wafadhili wajitokeza na kuwapiga jeki kwenye shughuli za kupalilia talanta za wachezaji wanaokuja.

”Tumegundua wapo chipukizi wengi wanaopania kunoa vipaji vyao na kuibuka wachezaji tajika humu nchini na kimataifa miaka ijayo lakini ufadhili ni donda sugu,” amesema na kuongeza kuwa itakuwa furaha kwao endapo watakuza wachezaji na kufaulu kuteuliwa kuchezea timu ya taifa bila kuweka katika kaburi sahau kushiriki voliboli ya kulipwa.

”Hatua ya kutuza wachezaji wanaofanya vizuri hutia wenzao motisha nao kutia bidii wakilenga kuwafikia wenzao,” alisema na kutoa wito kwa KVF iwe ikituza wachezaji wanaokuja.

Wachezaji wa Nyanza Prisons (kulia) wakiwakabili waopinzani wao. PICHA | JOHN KIMWERE

Nyanza Prisons inajumuisha: Leister Mudibo, Fredrick Ododa, Felix Oduor, Vitalis Wekesa, Kevin Wanjala, Chester Ongoro, Simon Omondi, Kevin Kimaru, Bernard Ochola, Kevin Muyelele, Walter Kipkurgat na Julius Wekesa. Pia wapo Joseph Murimi, Bethwel Rotich, Nicholas Njoroge, Manuel Ndiema, Victor Mutai, Kennedy Ondiek, Enock Kiprono, Dan Simiyu na William Odhiambo.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake 2,000 wahudhuria kikao cha Nyoro, waahidi sauti...

Maaskofu wahofia fujo uchaguzi ukitarajiwa 2023

T L