• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 8:50 AM
Maaskofu wahofia fujo uchaguzi ukitarajiwa 2023

Maaskofu wahofia fujo uchaguzi ukitarajiwa 2023

NA KITSEPILE NYATHI

HARARE, ZIMBABWE

MAASKOFU wa Kanisa Katoliki nchini Zimbabwe wameonya kwamba huenda uchaguzi mkuu wa mwaka 2023 ukakumbwa na ghasia ikiwa wadau hawatafanya mazungumzo.

Wametoa onyo hilo wakati ambapo taharuki inaendelea kupanda nchini humo kwa sababu ya kuzorota kwa uchumi na kudhulumiwa kwa wanasiasa wa upinzani.

Rais Emmerson Mnangagwa, anasaka nafasi ya kuendelea kuongoza kwa muhula wa tatu kupitia uchaguzi huo utakaofanyika 2023.

Aliingia mamlakani miaka mitano iliyopita baada ya wanajeshi kumwondoa mamlakani kiongozi wa muda mrefu wa Zimbabwe Robert Mugabe.

Lakini utawala wake umekashifiwa kwa kuwa dhalimu hata kuliko ule wa Dkt Mugabe huku uchumi wa nchi hiyo ukiporomoka kutokana na vikwazo iliyowekewa na Umoja wa Ulaya (EU).

Kwenye barua waliotoa Jumatatu, maaskofu hao walisema raia wengi wa Zimbabwe wanaishi maisha ya uchochole na “yasiyo ya utu”.

Walionya kwamba tayari joto la kisiasa nchini humo limeanza kupanda kwa sababu ya uchaguzi mkuu ukaofanyika mwaka ujao.

“Ghasia, umwagikaji wa damu na hali ya uhasama wa kisiasa imeanza kushuhudiwa nchini Zimbabwe kabla ya kufanyika kwa uchaguzi,” ikasema sehemu ya barua ya maaskofu hao.

“Kile kimefanya hali kuwa mbaya zaidi ni kudorora kwa uchumi wa nchi na kupanda kwa bei ya bidhaa za kimsingi. Raia wameshindwa kumudu bei ya hizi na huduma muhimu,” wakaongeza.

Mfumko wa bei nchini Zimbabwe umefikia kiwango cha asilimia 192 (kiwango cha juu zaidi duniani) kutokana na kuzorota kwa uchumi.

Kudorora kwa thamani ya sarafu ya Zimbabwe pia kumesababisha ongezeko la bei za bidhaa za kimsingi kama vile mafuta na mkate.

Hii ina maana kuwa raia wengi wa Zimbabwe wanapitia wakati mgumu kimaisha.

Maaskofu hao wa Kanisa Katoliki walisema kuwa sera za kisiasa na za kiuchumi za rais Mnangagwa zimefeli, hali ambayo imeibua uasi miongoni mwa raia.

“Ikiwa, kulingana na mafunzo ya Kanisa Katoliki, thamani ya sera hizo zitakadiriwa kwa misingi ya athari zao kwa watu maskini, hivyo ni sawa kusema kuwa sera zetu za kiuchumi na kisiasa zimefeli,” maaskofu hao wakaongeza.

“Umaskini umewaathiri zaidi watu wetu. Kwa hivyo, ili kuondoa changamoto zetu za kisiasa, kijamii na kiuchumi, kuna haja ya mazungumzo ya kina kufanywa nchini,” wakaongeza.

Viongozi hao wa kidini walisema ni makosa kwa serikali kudhani kuwa chama tawala pekee ndicho chenye suluhu kwa matatizo yanayokumba Zimbabwe.

“Kuna umuhimu wa vyama vyote vya kisiasa kufanya mazungumzo kuhusu njia za kukabiliana na shida zinazowakumba raia wa taifa letu,” maaskofu hao wakasema.

Rais Mnangangwa amekataa kufanya mazungumzo na mpinzani wake mkuu Nelson Chamisa tangu mwaka wa 2018, aliposhinda urais kwa kura chache.

Badala yake rais huyo ameamua kufanya mazungumzo na viongozi wa vyama vidogo vidogo vilivyoshiriki uchaguzi huo.

  • Tags

You can share this post!

Nyanza Prisons yajiwekea malengo ya kunyakua taji la...

Mang’u yang’aa katika mashindano ya somo la...

T L