• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
NYOTA WA WIKI: Bukayo Saka

NYOTA WA WIKI: Bukayo Saka

Na GEOFFREY ANENE

BUKAYO Saka ni mmoja wa wachezaji makinda wanaoendelea kuleta raha kambini mwa Arsenal FC, kiasi cha timu hiyo kuaminika kuwa na fursa kubwa ya kurejea Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Mchezaji huyo kwa jina la utani kama Sakinho, alipata mabao mawili katika mechi moja kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL); katika ushindi wa 5-0 ambao kikosi hicho, maarufu kama Gunners, kiliandikisha dhidi ya Norwich wiki moja iliyopita.

Kiungo huyo matata wa pembeni kulia, anayeweza pia kutumiwa kama beki wa pembeni kushoto ama winga, alifikisha idadi yake ya mabao ligini kuwa 10 katika mchuano huo akiwa na umri wa miaka 20 na siku 112.

Mabao hayo yalimfanya kuwa mchezaji wa pili mchanga zaidi wa Arsenal baada ya Nicolas Anelka, kuandikisha historia hiyo akiwa na miaka 19 na siku 225.

Saka pia ni mchezaji wa tatu mwenye umri mdogo kufunga bao Desemba 26 kwa miaka miwili mfululizo, baada ya Michael Owen (umri wa miaka 19 na siku 13) na Florent Sinama-Pongolle (miaka 20 na siku 67).

Kinda huyu alianza kufukuzia ndoto ya uanasoka kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Hata hivyo, alipiga hatua katika uchezaji wake alipojiunga na akademia ya Arsenal maarufu Hale End, akiwa na umri wa miaka minane.

Grafu yake imekuwa ikipanda tangu wakati huo, ingawa alinufaika pakubwa Aaron Ramsey na Alex Iwobi walipojiunga na Juventus na Everton mtawalia msimu 2018-2019, na pia akampiku kinda mwenzake Reiss Nelson kimchezo.

Weledi wa kusumbua uwanjani kwa kasi na chenga zake umechangia thamani yake ikapanda kufikia zaidi ya Sh8.0 bilioni.

Pia, mchezaji huyu mwenye asili ya Nigeria anaaminika kumezewa mate na miamba Liverpool.

Aidha, aliwahi kuwa kwenye rada ya Juventus na Atletico Madrid mapema msimu huu.

Baadhi ya vyombo vya habari barani Ulaya vinamweka Saka katika kiwango kimoja cha uchezaji na chipukizi matata Phil Foden (Manchester City), Joao Felix (Atletico Madrid), Kylian Mbappe (Paris Saint-Germain) na Erling Haaland (Borussia Dortmund).

Mchezaji huyu bora wa Arsenal msimu 2020-2021 anamuenzi sana raia wa Uswidi na winga matata wa zamani wa Arsenal, Freddie Ljungberg, kama shujaa wake.

Ljungberg alikuwa kocha wa chipukizi wa Arsenal nyota ya Saka ilipochomoza Hale End.

Kinda huyu alisaini kandarasi ya miaka minne na Arsenal mnamo Julai 2020. Gunners wanasemekana kuanza tayari mazungumzo kwa nia ya kuongeza kandarasi yake.

Kimataifa, Saka anawakilisha Uingereza. Alipoteza penalti katika fainali ya Kombe la Euro 2020 dhidi ya Italia iliyobeba taji.

You can share this post!

China yapiga marufuku matumizi ya chale miongoni mwa...

Mulembe wapiga jeki Raila kwa kuunga Azimio

T L