• Nairobi
  • Last Updated May 10th, 2024 3:33 PM
Mulembe wapiga jeki Raila kwa kuunga Azimio

Mulembe wapiga jeki Raila kwa kuunga Azimio

DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA

AZMA ya urais ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ilipigwa jeki Ijumaa baada ya viongozi kadha wa eneo la magharibi kutangaza watamuunga mkono kwenye uchaguzi wa mwaka huu 2022.

Katika hatua iliyoonekana kumwadhibu kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi, muungano wa jamii ya Waluhya ulimpokonya wadhifa wa msemaji wa jamii hiyo.

Walimkabidhi Gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya wadhifa huo ambao Bw Mudavadi ameushikilia tangu Desemba 31, 2016.

Bw Mudavadi alipata pigo zaidi baada ya naibu kiongozi wa ANC Ayub Savula na mbunge wa Teso Kaskazini Oku Kaunya kutangaza kugura muungano wa One Kenya Alliance (OKA) na kujiunga na vuguvugu la Azimio la Umoja.

Mkutano huo uliojulikana kama Bukhungu II, ulihudhuriwa na zaidi ya wabunge 30, maseneta kadha na magavana Oparanya, Wilbur Otichillo (Vihiga), James Ongwae (Kisii), Charity Ngilu (Kitui) na Sospeter Ojaamong (Busia).

Maafisa wakuu serikalini pia walihudhuria, miongoni mwao wakiwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa (Ulinzi), Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju, makatibu wa wizara Simon Nabukwesi (Elimu ya Juu), Bi Josephtha Mukobe (Idara ya Utamaduni) na Naibu Mkuu wa Utumishi wa Umma Wanyama Musyambo.

Wabunge, Mbw Savula na Kaunya walitumia jukwaa hilo kutangaza kuwa watampigia debe Bw Odinga katika eneo hilo la magharibi.

Bw Kaunya aliahidi kujiunga na ODM siku zijazo huku akimwalika Bw Odinga kuzuru kaunti ya Busia kuendeleza kampeni zake.

Bw Savula akasema: “Tuko na mirengo miwili ya kisiasa nchini Kenya. Uchaguzi wa 2022 ni mashindano ya farasi wawili ambao ni Raila na Naibu Rais William Ruto. Kwa sababu ya hali ya kuchanganyikiwa iliyoko katika OKA, nimeamua kugura na kujiunga na Azimio la Umoja chini ya Baba.”

Kwa upande wake, Bw Kaunya alisema alihudhuria mkutano huo kuandaa njia kwa kiongozi wa chama cha ANC Bw Mudavadi ili ajiunge na safari wa kumpeleka Bw Odinga Ikulu.

Wabunge wengine waliotangaza kujiunga na Azimio la Umoja ni pamoja na: kiranja wa wengi katika bunge la kitaifa Emmanuel Wangwe (Navakholo), Benard Shinali (Ikolomani), Dkt Simiyu Eseli (Tongaren), Wafula Wamunyinyi (Kanduyi) na Mbunge Maalum wa ANC Godfrey Osotsi.

Madiwani wapatao 10 waliochaguliwa kwa tiketi ya chama cha ANC katika kaunti za Kakamega, Bungoma na Vihiga pia walitangaza kujiunga na chama cha ODM, pamoja na vuguvugu la Azimio la Umoja.

Mkutano huo, maarufu kama Bukhungu II uliandaliwa na Katibu Mkuu wa Muungano wa Wafanyakazi Nchini (COTU) Francis Atwoli kutoa mwelekeo wa kisiasa kwa jamii ya Waluhya kuelekea uchaguzimkuu wa Agosti 9, 2022.

Akihutubu katika mkutano huo, Bw Atwoli alielezea furaha yake kwamba mkutano huo uliendelea bila vurugu na ukafikia lengo lake na kuunganisha eneo hilo.

Alisema eneo lote la magharibi mwa Kenya linaunga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja na kwamba litaunga mkono Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha urais.

Muungano wa Wazee wa Jamii ya Waluhya, unaowakilisha makabilwa madogo 18, yanayounda jamii hiyo, uliwasilisha maazimio matano.

Akisoma maazimio hayo Katibu Mkuu wa muungano huo Peter Ludava alisema lengo kuu la maazimio yao ni kuhakikisha kuwa wakazi wa eneo hilo wanampigia kura Bw Odinga.

You can share this post!

NYOTA WA WIKI: Bukayo Saka

Mudavadi na Wetang’ula wakwepa ‘mtego’ wa...

T L