• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:42 PM
Obiri atamalaki mbio za Cursa dels Nassos nchini Uhispania na kufunga mwaka wa 2020 kwa matao ya juu

Obiri atamalaki mbio za Cursa dels Nassos nchini Uhispania na kufunga mwaka wa 2020 kwa matao ya juu

Na CHRIS ADUNGO

MWANARIADHA Hellen Obiri alifunga mwaka wa 2020 kwa matao ya juu baada ya kuibuka mshindi wa mbio za kilomita 10 za Cursa dels Nassos mnamo Disemba 31, 2020.

Bingwa huyo wa dunia katika mbio za mita 5,000 alikamilisha mbio za Cursa dels Nassos zilizoandaliwa jijini Barcelona, Uhispania baada ya muda wa dakika 30:53.

Obiri ambaye pia ni bingwa dunia katika mbio za nyika alijinyanyua licha ya kuanguka katika kilomita moja ya mwisho na kuwapiku raia wa Ethiopia Majida Maayouf (33:19) na Marta Galimany (33:52).

Mkenya mwingine, Daniel Simiu alitawala mbio za kilomita 10 za San Silvestre jijini Madrid, Uhispania mnamo Disemba 31.

Mtimkaji huyo alifika utepeni akiwa wa kwanza kwa muda wa dakika 27:41 baada ya kuwazidi maarifa Faniel Eyob wa Italia (28:08) na Mkenya raia wa Amerika ambaye pia ni bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 5,000 Paul Chelimo (28:14).

Yalemzerf Yahualaw wa Ethiopia alitamalaki mbio hizo za San Silvestre kwa upande wa wanawake baada ya kukata utepe kwa dakika 31:17. Bingwa wa dunia katika marathon, Mkenya Ruth Chepng’etich aliambulia nafasi ya pili (31:50) mbele ya Alesia Zarbo wa Ufaransa aliyesajili muda wa dakika 33:00 na kuridhika na nafasi ya tatu.

Katika mbio za kilomita 10 za Boclassic zilizoandaliwa mjini Bolzano, Italia, mshindi wa nishani ya shaba katika mbio za mita 5,000 duniani, Margaret Chelimo aliibuka mshindi.

Chelimo aliandikisha muda wa dakika 30:42 na kumbwaga Mkenya mwenzake, Dorcas Jepchirchir aliyepigiwa upatu wa kuwika baada ya kuambulia pakavu kwenye nusu marathon ya dunia jijini Gydnia, Poland na Valencia Half Marathon nchini Uhispania mnamo Oktoba na Disemba 2020 mtawalia.

Jepchirchir aliambulia nafasi ya pili kwa muda wa dakika 30:43 mbele ya Mkenya raia wa Kazakhstan, Norah Jeruto (30:46).

Wakenya Gloria Kite na Janet Kisa walifunga orodha ya wanariadha watano wa kwanza baada ya kuambulia nafasi za nne na tano kwa muda wa dakika 32:26 na 33:03 mtawalia.

You can share this post!

Watford wajinasia fowadi matata kutoka Ligi Kuu ya Norway

Covid-19 yaunyima mwaka 2021 makaribisho ya haiba