• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Obiri, Brigid wala sifa kedekede Siku ya Wanawake Duniani

Obiri, Brigid wala sifa kedekede Siku ya Wanawake Duniani

Na GEOFFREY ANENE

MAMA wa Taifa Margaret Kenyatta amewasherehekea wanariadha wa kike nchini kwa kupeperusha juu bendera ya Kenya ulimwenguni kote, kudumisha bidii na uvumilivu siku zote, na pia kujitolea kuifaa jamii kupitia miradi mbalimbali.

Akiadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake hapo Jumatatu, Mama wa Taifa alisema Kenya imeshuhudia ongezeko la wanariadha bora wa kike, waliopata ufanisi mkubwa na kuweka rekodi nyingi mpya duniani baada ya kushinda vizuizi.

“Tumeshuhudia juhudi zao katika kuwafungulia wanawake na wasichana wengine nafasi ya kufuata nyayo zao na kuwainulia kiwango, kupitia kwao kuwa mifano bora na walezi shupavu,” alisema Bi Kenyatta kupitia mtandao wa YouTube katika ujumbe wake kwa Shirikisho la Riadha Duniani (WA), ambalo limekuwa likiwaenzi wanawake wanariadha mwezi huu wa Machi kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake.

Mama wa Taifa pia alieleza umuhimu wa michezo kuwa moja kati ya majukwaa bora ya kukuza usawa wa kijinsia pamoja na kuinua wanawake na wasichana katika jamii.

“Hii ndio maana Shirikisho la Riadha Duniani (WA) liliazimia kuwasherehekea wanawake wanariadha wiki ambayo ni ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake,” akasema.

Aliwataja wanariadha mashuhuri wa kike, kama vile Tegla Loroupe na Catherine Ndereba, kama mfano bora kwani walibobea na kuhakikisha wanaacha urithi wa kudumu katika riadha.

Loroupe ni bingwa wa zamani wa marathon za kifahari za London, Berlin na New York; naye Ndereba ni mshindi mara mbili wa medali ya fedha katika fani hiyo ya mbio za kilomita 42 kwenye Olimpiki.

Loroupe alianzisha Wakfu wa Amani wa Tegla Loroupe mwaka 2003 kusaidia kuleta amani na utangamano kati ya jamii za Pokot na Turkana.

Kwa upande wake, Ndereba amejitolea kufundisha na kukuza talanta katika Idara ya Magereza nchini.

Aidha, Mama wa Taifa alimtambua bingwa mara mbili wa London na Chicago Marathon – Brigid Kosgei, 27, anayeshikilia rekodi ya dunia ya mbio za marathon kwa sasa.

Alipongeza pia wanariadha wengine mashuhuri wakiwemo Peres Jepchirchir, Hellen Obiri na Faith Kipyegon.

Obiri ndiye bingwa wa dunia katika mbio za 5000m, akitetea taji hilo mnamo 2019 wakati wa Mashindano ya Riadha Duniani ya IAAF jijini Doha, Qatar.

Bi Kenyatta alisema wanariadha hao wameendelea kuwa kielelezo bora kwa wasichana na wanawake wengi ambao wanaanza taaluma yao ya riadha shuleni na kambi za mafunzo nchini.

Akitoa mfano wa mbio za Beyond Zero Half Marathon, Bi Kenyatta alisema fedha pamoja na kampeni ya hamasisho zimesaidia katika miradi ambayo imechangia pakubwa kupunguza vifo vya akinamama wajawazito, kumaliza ukeketaji, ndoa za mapema na maambukizi mapya ya HIV nchini.

You can share this post!

VITUKO: Munira na walimu wachache wapanga kuwapunja wenzao...

Mashabiki wa Kenya kukosa Olimpiki baada ya Japan kupiga...