• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:40 PM
Obiri mawindoni Istanbul Half Marathon, Kwemoi akivumisha kitengo cha wanaume

Obiri mawindoni Istanbul Half Marathon, Kwemoi akivumisha kitengo cha wanaume

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA Hellen Obiri yuko katika orodha ya wakimbiaji 8,000 wanaowinda taji kwenye makala ya tisa ya Istanbul Half Marathon nchini Uturuki leo Jumapili.

Obiri, 32, ameshiriki mbio tatu za umbali huo wa kilomita 21 akimaliza Istanbul Half Marathon (Uturuki) na Ras Al Khaimah (Milki za Kiarabu) katika nafasi ya pili kwa saa 1:04:51 na 1:04:22 mtawalia na kutwaa ushindi wa Great North Run nchini Uingereza kwa 1:07:48.

Katika shindano lake la nne, Mkenya huyo ameeleza vyombo vya habari Istanbul kuwa analenga kuimarisha muda wake bora wa 1:04:22.

“Hali ya anga ikiwa nzuri na pia wawekaji kasi wakifanya kazi vyema, basi nitajaribu kuvunja muda wangu bora. Lengo ninapoingia mashindano kama haya ni kujaribu kukimbia vyema na kuimarisha muda wangu,” alisema Ijumaa. Aliongeza kuwa yuko katika hali nzuri kuliko alivyokuwa Ras Al Khaimah mwezi uliopita.

Alipoulizwa iwapo anaweza kuvizia rekodi ya Istanbul Half Marathon ya kinadada ya 1:04:02 inayoshikiliwa na mshindi wa 2021 Ruth Chepng’etich kutoka Kenya, alisema, “Hiyo ni kibarua kigumu. Hata hivyo, kuna watimkaji matata hapa kwa hivyo hatutasita kujaribu kuifuta.”

Wapinzani wake wakuu wanatoka Ethiopia na Uturuki pamoja na Wakenya Vicoty Chepngeno, Pauline Esikon, Daisy Kimeli na Ludwina Chepngetich. Vicoty ameshinda nusu-marathon 11 kati ya 14 ameshiriki nusu-marathon kwa hivyo ni tishio kubwa.

Rekodi ya wanaume ya Istanbul ya dakika 59:35 inayoshikiliwa na Kibiwott Kandie itakuwa hatarini kuvunjwa baada ya Wakenya wenzake Daniel Mateiko (58:26) na Rodgers Kwemoi (58:30) kuapa kuivizia. Wakenya wengine hapa ni Josphat Tanui (59:22), Edmond Kipngetich (59:41), Hillary Kipchumba (60:01), Vestus Chemjor (60:47), Moses Too (60:56), Philimon Kiptoo (61:47), Daniel Kiprotich (62:09) na Gerald Vincent (62:27).

You can share this post!

Ruto alia anafinywa na serikali

Ujerumani yazamisha Israel na kuendeleza rekodi ya...

T L