• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
Ruto alia anafinywa na serikali

Ruto alia anafinywa na serikali

ONYANGO K’ONYANGO Na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais Dkt William Ruto amelalamikia kile ambacho anadai ni afisi yake kunyimwa pesa kutoka kwa Hazina Kuu ya Kitaifa.

Vile vile, Dkt Ruto anasema chama cha Jubilee kinatumia mamilioni ya pesa kushawishi wafuasi wa chama chake cha United Democratic Alliance (UDA) wakihame.

Kulingana na duru kutoka afisi yake, Dkt Ruto amekuwa akitumia pesa zake binafsi kugharimia mahitaji ya wafanyakazi wake wanaoandamana naye katika ziara za kampeni kote nchini baada ya afisi yake kunyimwa pesa.

Mfanyakazi wake mmoja alisema mhasibu katika Afisi ya Rais amekataa kuidhinisha malipo ya kugharimia usafiri wa wafanyakazi wa Afisi ya Naibu Rais.

Pia, alifichua kuwa, Dkt Ruto hujaza mafuta kwenye magari ya serikali anayotumia katika kampeni zake kwa sababu hapokei tena pesa kama hapo awali kwa shughuli hiyo.

Madai hayo yanakuja baada ya aliyekuwa mwaniaji wa Urais mnamo 2017 Dkt Ekuru Aukot hivi majuzi kuandikia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC), akidai Dkt Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga wamekuwa wakitumia fedha za walipa kodi katika kampeni zao.

Dkt Aukot alisema kuwa Dkt Ruto amegeuza makao ya Naibu Rais mtaani mtaani Karen kama kituo cha kampeni kwa kuwa amekuwa akiwapokea wanasiasa wanaoguria kambi yake.

Pia kuwa kampeni za Bw Odinga chini ya vuguvugu la Azimio la Umoja zimekuwa zikifadhiliwa na pesa za walipaji ushuru ikizingatiwa anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta.

Mkurugenzi wa Mawasiliano katika Afisi ya Naibu Rais Emmanuel Talam, alifafanua kuwa serikali ilisitisha ufadhili kwa shughuli rasmi za afisi hiyo mnamo Septemba 2021 bila ufafanuzi wowote.

“Idara zote katika afisi ya Naibu Rais hazijapokea pesa kutoka kwa Hazina ya kitaifa na tumeambiwa inaathiri serikali yote. Afisi hiyo imefanya mipango kivyake ili shughuli zisisambaratishwe. Hata hivyo, wafanyakazi wamekuwa wakipokea mshahara wao kama kawaida kutoka kwa serikali,” akasema Talam.

Duru katika Afisa ya Dkt Ruto zilimlimbikizia lawama msimamizi wa Ikulu Kinuthia Mbugua, wakidai ndiye alisababisha ufadhili huo kukatizwa.

“Bajeti ya Afisi ya Rais inahusisha Rais na Naibu Rais. Serikali haifadhili tena gharama ya mafuta kwenye magari yanayotumiwa na Naibu Rais. Bajeti huwa inaidhinishwa na msimamizi wa Ikulu Kinuthia Mbugua ambaye haruhusu magari ya Dkt Ruto yajazwe mafuta kwenye vituo vya mafuta vya National Oil kama zamani,” ziliarifu duru hizo.

Haya yanajiri huku washirika wa Dkt Ruto wakilalamika kuwa serikali inatumia rasilmali za serikali kufadhili kampeni za muungano wa Azimio la Umoja.

Wakizungumza wakiwa Naivasha Ijumaa, wanasiasa hao walisema ni makosa kwa serikali kutumia pesa za umma kwa kampeni.

Kauli zao zinachukuliwa kama hasira baada ya serikali kuchukua hatua za kukausha mifereji ya pesa za kampeni ya Dkt Ruto.

“Tunajua kwamba, njia ambazo Dkt Ruto alikuwa akifadhili kampeni zake zimefungwa na washirika wake pia wameishiwa. Hii ndiyo sababu anadai anafinywa ilhali ni makosa kutumia rasilmali za serikali kufanya kampeni,” alisema mdadisi wa siasa, Peterson Oloo.

Oloo anasema kwa miaka minne, serikali ilimuacha Dkt Ruto kutumia mali ya umma kujipigia debe na inapochukua hatua lazima ahisi uchungu.

Dkt Ruto amekuwa akilalamika kuwa washirika wake wamekuwa wakihangaishwa na serikali ikiwa ni pamoja na kushtakiwa na kufungiwa akaunti za benki.

Washirika wa Dkt Ruto vile vile wanalalamika kuwa, chama tawala cha Jubilee kimekuwa kikitumia pesa kuwanunua wanasiasa wakihame.

Wanasiasa hao wanadai kwamba, baadhi ya wanaokataa ushawishi wamekuwa wakitishwa.

You can share this post!

Equator Rally yavutia madereva 23 Jeremy Wahome akirejea...

Obiri mawindoni Istanbul Half Marathon, Kwemoi akivumisha...

T L