• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Olunga butu Harambee Stars ikiona vimulimuli dhidi ya Mali

Olunga butu Harambee Stars ikiona vimulimuli dhidi ya Mali

Na GEOFFREY ANENE

MSHAMBULIAJI matata Michael Olunga alikuwa butu timu ya Harambee Stars ikibebeshwa na Mali magoli 5-0 katika mechi yake ya tatu ya Kundi E ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Wenyeji Mali, ambao walialika Kenya jijini Agadir nchini Morocco kwa sababu viwanja vyao havijafikia viwango vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), walizamisha Stars kupitia kwa mabao ya Ibrahim Kone (matatu), Adama Traore na Moussa Doumbia.

Nahodha Olunga, ambaye amekuwa akifanya makubwa katika klabu yake ya Al Duhail nchini Qatar ikiwemo kufunga mabao matano dhidi ya Al Sailiya 5-0, alitarajiwa kuonyesha fomu hiyo yake.

Hata hivyo, Stars haikuwa na lake katika mchuano huo ambao mvua ya magoli ilianza kunyesha dakika ya saba kupitia Traore. Kone aliongeza mabao matatu kabla ya mapumziko ikiwemo penalti dakika ya 45. Doumbia alihitimisha dakika ya 85.

Mashabiki wa Kenya wamekejeli Stars na viongozi Shirikisho la Soka Kenya (FKF) kwa matokeo hayo yanayozima matumaini ya vijana wa kocha Engin Firat kunyakua tiketi moja iliyo mezani ya kuingia awamu ijayo.

“Uchungu ambao mmetusababishia hatuwezi hata kuueleza,” shabiki Owuor Owuor alisema akielezea masikitiko ambayo mashabiki wamepata.

Mali inaongoza kundi hilo kwa alama saba ikifuatiwa na Uganda (tano), Kenya (mbili) na Rwanda (moja). Uganda ilipepeta Rwanda 1-0 jijini Kigali.

Stars tayari imefunga safari ya kurejea Nairobi kwa mechi ya marudiano dhidi ya Mali itakayosakatwa Oktoba 10 ugani Nyayo.

Katika matokeo mengine ya Alhamisi, Liberia ililemewa 2-1 na Cape Verde jijini Accra nchini Ghana, DR Congo ikapepeta Madagascar 2-0 (Kinshasa), Tanzania ikachapwa 1-0 na Benin (Dar es Salaam), Equatorial Guinea ikapiga Zambia 2-0 (Malabo), Nigeria ikaduwazwa 1-0 na Jamhuri ya Afrika ya Kati (Lagos) nayo Tunisia ikazaba Mauritania 3-0 mjini Rades.

Tunisia inaongoza Kundi B kwa alama tisa ikifuatiwa na Equatorial Guinea (sita), Zambia (tatu) na Mauritania (sifuri).

Super Eagles ya Nigeria inasalia kileleni mwa Kundi C kwa alama sita ikifuatiwa na Cape Verde na Jamhuri ya Afrika ya Kati (nne kila moja) na Liberia (tatu).

Benin imekaa juu ya Kundi J kwa alama saba, mbili mbele ya DR Congo nayo Tanzania imezoa alama nne. Madagascar inapatikana mkiani bila alama. Washindi wa makundi yote 10 wataingia awamu ya muondoano. Droo ya awamu hiyo itakutanisha mataifa mawili mawili ambapo washindi watajikatia tiketi ya kuwa Qatar mwaka 2022.

Kikosi cha Harambee Stars kilichosafiri Morocco:

Makipa – Ian Otieno, Brian Bwire, Faruk Shikhalo;

Mabeki – Joseph Okumu, Joash Onyango, David Owino Odhiambo, Johnstone Omurwa, Eugene Asike, Daniel Sakari, David Owino Ambulu, Abud Omar, Eric Ouma, Bolton Omwenga;

Viungo – Richard Odada, Lawrence Juma, Ismael Gonzalez, Kenneth Muguna, Duke Abuya, Boniface Muchiri, Eric Zakayo, Phillip Mayaka, Abdalla Hassan;

Washambuliaji – Michael Olunga, Henry Meja, Eric Kapaito.

You can share this post!

Ngilu aagizwa afike kortini kueleza sababu ya kutolipa...

Jubilee kuachia kila raia deni la Sh180,000