• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Ongwae kuhama Bears nchini Denmark baada ya kuichezea miaka mitatu

Ongwae kuhama Bears nchini Denmark baada ya kuichezea miaka mitatu

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa mpira wa vikapu nchini Kenya, Tylor Okari Ongwae anataka kuhama mabingwa wa Denmark, Bakken Bears Aarhus baada ya kuwa nao miaka mitatu.

Ongwae ameshinda Ligi Kuu akichezea Bears msimu 2018-2019, 2019-2020 na 2020-2021 pamoja mataji mawili ya Kombe la Denmark msimu 2019-2020 na 2020-2021.

Mkenya huyo, ambaye atasherehekea kufikisha umri wa miaka 30 hapo Julai 15, pia amechezea Bears kwenye Klabu Bingwa Ulaya pamoja na mashindano ya daraja ya pili barani Ulaya, Europe Cup.

“Hatuna habari kuhusu Tylor. Tungependa aendelee kuwa mchezaji wetu mjini Aarhus, lakini kwa sasa anataka kuangalia kama kuna klabu nyingine mbadala,” mkurugenzi wa michezo wa Bakken Bears, Michael Piloz aliambia Taifa Leo katika mahojiano baada ya klabu hiyo kutangaza kupata kocha mpya Anders Sommer mnamo Jumatano.

Mbali na Bears, Ongwae amecheza mpira wa vikapu katika chuo cha Ranger Junior na Chuo Kikuu cha Louisiana nchini Amerika, klabu ya Felice nchini Italia, Solna Vikings na Sodertalje nchini Uswidi, Taranaki nchini New Zealand na Massagno nchini Uswizi kabla ya kujiunga na Bears mwaka 2018 ukielekea kutamatika.

Nyota huyo alisaidia Kenya kuingia Kombe la Afrika (AfroBasket) kwa mara ya kwanza tangu 1993 alipofunga alama mbili za mwisho sekunde ya mwisho katika ushindi wa 74-73 dhidi ya miamba Angola mwezi Februari 2020. Atakuwa muhimu katika kampeni za Kenya katika dimba hilo litakalofanyika nchini Rwanda mnamo Agosti 25 hadi Septemba 5.

  • Tags

You can share this post!

Masika na Vissel Kobe wanyeshea Suzuka Point Getters kipute...

Kenya yapoteza fursa kuandaa mashindano ya mpira wa vikapu...