• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 6:39 PM
Pele afanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe wa utumbo

Pele afanyiwa upasuaji kuondoa uvimbe wa utumbo

Na MASHIRIKA

JAGINA wa soka kutoka Brazil, Pele, amefanyiwa upasuaji wa kuondoa uvimbe kwenye utumbo baada ya kulazwa hospitalini kwa siku sita.

“Nina bahati ya kusherehekea ushindi wa Brazil katika mechi muhimu nikiwa mzima. Sasa nitatazama mechi yenu ijayo ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nikitabasamu,” akasema mshindi huyo mara tatu wa Kombe la Dunia.

Siku tano zilizopita, Pele ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Santos na New York Cosmos alikana ripoti kwamba alianguka chini na kuzimia kabla ya kufikishwa hospitalini kwa matibabu.

Mnamo Februari 2020, Edinho ambaye ni mwanawe Pele na kipa wa zamani wa Santos, alikiri kwamba baba yake mzazi alikuwa na aibu ya kutoka nje ya nyumba kwa sababu asingeweza kutembea bila ya usaidizi.

Afya ya nguli huyo ni suala ambalo limezungumziwa mno na vyombo vya habari nchini Brazil tangu afanyiwe upasuaji mwingine mnamo 2015 baada ya kulazwa hopsitalini kwa mara ya pili chini ya kipindi cha miezi sita. Afya yake ilidorora tena mnamo 2019 na akalazwa hospitalini kwa wiki mbili.

Pele ndiye mfungaji bora wa muda wote nchini Brazil na ni miongoni mwa wanasoka wanne pekee kuwahi kufunga bao katika fainali nne tofauti za Kombe la Dunia.

Kwa mujibu wa Guinness Book of World Records, Pele aliwahi kufunga mabao 1,279 kutokana na mechi 1,363 katika enzi zake kitaaluma. Kati ya mabao hayo ni 77 aliyofungia Brazil katika mechi 91 za kimataifa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Makala ya michezo: Winga na nahodha ambaye ameongeza...

TAHARIRI: Serikali iviondoe vizingiti vya CBC