• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 10:50 AM
Pigo kwa Man-United na PSG baada ya Juventus kufichua kwamba Ronaldo haendi popote

Pigo kwa Man-United na PSG baada ya Juventus kufichua kwamba Ronaldo haendi popote

Na MASHIRIKA

JUVENTUS wamesisitiza kwamba nyota Cristiano Ronaldo hajawasilisha ombi la kutaka kuagana nao, ungamo ambalo ni pigo kwa Manchester United na Paris Saint-Germain (PSG) ambao pia wanahemea maarifa yake.

Ronaldo, 36, amekuwa akihusishwa na uwezekano mkubwa wa kujiengua na Juventus baada ya kujiunga na kikosi hicho miaka mitatu iliyopita akitokea Real Madrid.

Licha ya kujivunia huduma za Ronaldo ambaye ni miongoni mwa wachezaji bora zaidi duniani kwa sasa, Juventus walishindwa kuhifadhi ufalme wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2020-21. Taji hilo lilinyakuliwa na Inter Milan walioongozwa na kocha Antonio Conte kulitia kapuni kwa mara ya kwanza tangu 2009-10.

Akijivunia tayari kufanya kazi chini ya wakufunzi watatu, kambini mwa Juventus, ilitarajiwa kwamba Ronaldo angekuwa radhi kuondoka baada ya Man-United na PSG kufichua maazimio ya kumsajili.

Hata hivyo, matumaini ya Man-United sasa kumsajili upya Ronaldo yamedidimia baada ya kumtwaa kiungo mvamizi raia wa Uingereza, Jadon Sancho kutoka Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa Sh12 bilioni.

PSG walikuwa wakiwania huduma za Ronaldo kwa matarajio kwamba angewasaidia kurejesha taji la Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) walilopokonywa na Lille mnamo 2020-21 pamoja na kujitwalia ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Italia, kikosi chochote ambacho kiko radhi kuweka mezani angalau Sh3.9 bilioni kwa sasa kina uwezo wa kujinasia maarifa ya Ronaldo kutoka Juventus.

Ingawa hivyo, afisa mkuu mtendaji wa Juventus, Federico Cherubini, amesisitiza kwamba ni matamanio yake kushuhudia Ronaldo akistaafu kwenye ulingo wa soka akiwa mchezaji wa Juventus.

Kufikia sasa, Ronaldo amefungia Juventus jumla ya mabao 101 kutokana na mechi 133.

Iwapo atasalia Juventus, basi Ronaldo ataungana upya na kocha wake wa zamani Massimiliano Allegri ambaye alirejea jijini Turin kujaza pengo lililoachwa na Andrea Pirlo aliyetimuliwa na Juventus mwishoni mwa msimu wa 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MATHEKA: Kuahirisha uchaguzi mkuu wa 2022 ni kukiuka Katiba

Cristiano Ronaldo aongoza kwa umaarufu kwenye Instagram