• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
MATHEKA: Kuahirisha uchaguzi mkuu wa 2022 ni kukiuka Katiba

MATHEKA: Kuahirisha uchaguzi mkuu wa 2022 ni kukiuka Katiba

Na BENSON MATHEKA

KUMEKUWA na mapendekezo kwamba uchaguzi mkuu wa mwaka ujao uahirishwe, ili kutoa nafasi ya kura ya maamuzi kupitia Mpango wa Maridhiano (BBI).

Katiba ya Kenya inasema kuwa uchaguzi mkuu unafaa kufanyika Agosti 9 mwaka ujao.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) tayari imeshatoa mipango yake ya kuandaa kura tarehe hiyo.

Kulingana na wanaopendekeza uchaguzi huo uahirishwe, mchakato wa kubadilisha Katiba ni muhimu kwa nchi hivi kwamba, kura inaweza kuahirishwa kwa mwaka mmoja au miwili hadi referenda ifanyike.

Mmoja wa waliotoa mapendekezo hayo ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Cotu), Francis Atwoli, aliyeashiria kuwa bila BBI kutekelezwa, uchaguzi mkuu hautafanyika mwaka ujao.

Wanachomaanisha ni kwamba sehemu ya Katiba inayosema kura lazima iandaliwe kila baada ya miaka mitano, isimamishwe kwa muda.

Huu ni msimamo unaofaa kukataliwa na Wakenya wote kwani unaenda kinyume na Katiba ya nchi.

Wakenya wana kila sababu ya kushawishika kuwa, hawa wanaotaka uchaguzi uahirishwe wako na nia fiche ambayo wanataka kuitimiza kupitia BBI, na bila shaka haiwezi kuwa kwa manufaa ya mwananchi wa kawaida.

Sio kwamba baadhi ya mapendekezo katika Mswada wa Marekebisho ya Katiba wa 2020 ni mabaya.

Kuna mambo mazuri katika mswada huo wa BBI, lakini kuna mengine yanayoweza kutumiwa na baadhi ya viongozi kujinufaisha.

Imetendeka katika mataifa mengine ambapo wanasiasa wametumia raia wao kubadilisha Katiba kisha wanatumia mageuzi hayo kuwakadamiza.

Inatia moyo kuona kuwa viongozi wa kidini na wanaharakati wamepinga vikali gumzo hilo la kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu.

Pingamizi hilo halijawafurahisha baadhi ya viongozi wanaounga marekebisho ya Katiba.

Wakenya wanafaa kuungana na viongozi wa kidini na wale wanaopinga kuahirishwa kwa kura.

Kulingana na Katiba, uchaguzi mkuu unaweza kuahirishwa Kenya ikiwa tu taifa liko katika vita; ambapo hoja hiyo itaidhinishwa tu iwapo mabunge yote mawili – Bunge la Kitaifa na Seneti – yataipitisha kwa thuluthi mbili ya wabunge wote.

Ikipitisha, uchaguzi unafaa kuahirishwa kwa muda wa miezi sita pekee wala si mwaka au miaka miwili kama walivyopendekeza Atwoli na wenzake.

Kwa kila hali, kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu kutokana na sababu zingine isipokuwa zilizotajwa kwenye Katiba, ni kukiuka Katiba ya nchi.

Wanaotoa pendekezo hilo wanafaa kusoma historia kufahamu yaliyotendeka katika nchi zilizoahirisha uchaguzi ili kutimiza maslahi ya watu wachache.

You can share this post!

Waliofungwa jela maisha kwa kuficha gaidi wa al-Qaeda...

Pigo kwa Man-United na PSG baada ya Juventus kufichua...