• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Pigo kwa Spurs jeraha la goti likitarajiwa kumweka mkekani kipa Hugo Lloris kwa wiki nane zijazo

Pigo kwa Spurs jeraha la goti likitarajiwa kumweka mkekani kipa Hugo Lloris kwa wiki nane zijazo

Na MASHIRIKA

KIPA na nahodha wa Tottenham Hotspur, Hugo Lloris, 36, atasalia mkekani kwa kipindi cha wiki sita au nane zijazo kuuguza jeraha la goti.

Nahodha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, aliumia wakati wa mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyoshuhudia waajiri wake Spurs wakizaba Manchester City 1-0 ugani Tottenham Hotspur mnamo Februari 5, 2023.

Kujeruhiwa kwa Lloris ni pigo kubwa kwa Spurs ambao sasa watalazimika kutegemea zaidi maarifa ya kipa wa zamani wa Southampton na timu ya taifa ya Uingereza, Fraser Forster.

Walinda-lango wengine kambini mwa Spurs ni Brandon Austin na Alfie Whiteman ambao ni makinda wa akademia wasio na tajriba.

Spurs kwa sasa wanakamata nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la EPL na wanawania nafasi ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu uhao.

 Watavaana na Leicester City ligini mnamo Februari 11, 2023 kabla ya kuwaendea AC Milan ya Italia katika mkondo wa kwanza wa hatua ya 16-bora ya UEFA msimu huu wa 2022-23 mnamo Februari 14, 2023.

Forster, aliyejiunga na Spurs mwishoni mwa msimu wa 2021-22 bila ada yoyote, amechezea kikosi hicho mara moja pekee – mechi iliyowakutanisha na Brentford mnamo Disemba 26, 2022 na kukamilika kwa sare ya 2-2.

Lloris aliyevalia utepe wa unahodha kwenye fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar, alistaafu soka ya kimataifa mnamo Januari 2023 baada ya Ufaransa kufungwa penalti 4-2 na Argentina kwenye fainali kufuatia sare ya 3-3. Aliongoza Ufaransa kupepeta Croatia 4-2 mnamo 2018 nchini Urusi na kujizolea ufalme wa Kombe la Dunia.

Kipa huyo hajafungwa bao katika mechi saba kati ya 21 kwenye EPL msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Koome: Polisi wetu hawakuenda kwa Matiang’i

Alexis Sanchez aongoza Olympique Marseille kung’oa...

T L