• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Pigo mkali wa Safari Rally akifariki

Pigo mkali wa Safari Rally akifariki

NA RICHARD MAOSI

IMEKUWA ni wiki ya simanzi kwa wanamichezo wa Mashindano ya Magari, baada ya kumpoteza mmoja wao, Arthur Kinyanjui ambaye alikuwa akitambulika kwa jina la utani kama AK47.

Kinyanjui alikuwa amelazwa katika hospitali ya Aga Khan jijini Mombasa alipokuwa akiendelea kupokea matibabu mpaka alipopoteza maisha yake mapema wiki hii.

Taifa Leo ilitembelea nyumbani kwao eneo la Bahati Nakuru, siku ya Jumanne na kushuhudia maandalizi ya mazishi, ambapo marehemu atapumzishwa wiki ijayo.

Kulingana na msemaji wa familia, Kinyanjui alikuwa ni mwanamichezo shupavu wa kuyaendesha magari ya Safari Rally ndani na nje ya Kenya.

Katika umri mdogo Kinyanjui alikuwa akiendesha gari aina ya Subaru Imprezza WRX, dhidi ya madereva mahiri kama vile Ian Duncun kwenye Mashindano ya Kimataifa ya Kenya National Autocross Championship(KNAC).

Aidha mnano mwaka wa 2009 alikuwa wa tatu kwenye mashindano ya Safari Rally, hatimaye miaka miwili baadaye alishiriki kwenye mashindano ya KCB Safari Rally na kufanya vyema.

“Februari mwaka huu Naibu wa Rais Dkt William Samoei Ruto, akiandamana na wanasiasa wa mrengo wa Tangatanga walimtembelea Kinyanjui, akiendelea kutibiwa mjini Mombasa,”akasema.

Kinyanjui ambaye ni mtoto wa mbunge wa Bahati Kimani Ngunjiri alikuwa ni umri wa miaka 32.

Kupitia mtandao wake wa kijamii Ngunjiri alieleza huzuni wake, akisema kuwa hakuamini kuwa alikuwa amempoteza mtoto wake ambaye alikuwa ni kitinda mimba.

You can share this post!

Mtambue mtangazaji wa soka chipukizi ‘Arocho’

Timu ya Viziwi Nakuru yajiandaa kwa mashindano ya Afrika