• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 5:30 PM
Pogba kusakata Kombe la Dunia

Pogba kusakata Kombe la Dunia

NA MASHIRIKA

TURIN, Italia

KIUNGO wa kimataifa, Paul Pogba hatahitaji upasuaji kutokana na jeraha la goti, na anatarajiwa kurudi uwanjani kuchezea Juventus kwa muda usio mrefu.

Kumekuwa na hofu kwamba nyota huyo mwenye umri wa miaka 29 angekosa fainali za Kombe la Dunia iwapo angefanyiwa upasuaji.

Akiwa kwenye kiwango cha juu, Pogba aliisaidia Ufaransa kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018, na ni majuzi tu aliporejea katika klabu ya Juventus kama mchezaji huru baada ya mkataba wake na Manchester United kumalizika.

Pogba alipata jeraha hilo mazoezini nchini Amerika akiwa kwenye kikosi cha vigogo hao wa Serie A.

Alikuwa kwenye timu iliyocheza na Chivas Guadalajara mwezi Julai, lakini alilalamika kwamba goti lake lilikuwa na machungu.

Lakini habari za hivi punde za La Gazzetta dello Sport zimeeleza kwamba mchezaji huyo ataendelea kutibiwa huku akifanya mazoezi ya viungo ambayo yatachukua wiki tano.

Juventus wataanza msimu kwa mechi ya Serie A dhidi ya Sassuolo nyumbani mnamo Jumatatu, Agosti 15 usiku.

Wakati huo huo, kipa Dean Henderson ameeleza maisha yake pale Old Trafford kama uhalifu mkubwa.

Mlinda lango huyo wa kimataifa mwenye umri wa miaka 25, alijiunga na Nottingham Forest kwa mkataba wa kudumu baada ya David de Gea kutegemewa kila wakati.

Henderson alisema angecheza mechi nyingi msimu uliopita, lakini jeraha lilimtatiza kiasi cha kukosa michuano ya Euro 2020, mbali na wakati mmoja kuambukizwa ugonjwa wa Covid-19 mara tu msimu ulipoanza rasmi.

Kipa huyo amelalamika kwa kupuuzwa huku akiongeza kwamba hajazungumza na kocha mpya Erik ten Hag tangu awasili mwezi Mei.

“Kwa hakika yalikuwa maisha magumu ya miezi 12 maishani mwangu,” akasema Henderson.

You can share this post!

KINYUA BIN KING’ORI: Viongozi na raia wahubiri amani...

Dosari za uchaguzi zatajwa kuwa tisho

T L