• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:55 AM
Prisons Mombasa yajipatia miaka mitatu kushiriki kipute cha CAVB

Prisons Mombasa yajipatia miaka mitatu kushiriki kipute cha CAVB

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya wanaume ya Maafande wa Prisons Mombasa ni kati ya vikosi 16 vinavyoshiriki kipute cha Ligi Kuu ya Voliboli nchini muhula huu. Prisons Mombasa iliasisiwa mwaka 2002 lakini ilianza kushiriki kampeni za kipute hicho mwaka 2010.

Kufuatia ushindani unaozidi kushuhudiwa kwenye kampeni za muhula huu kocha wake mkuu, Henry Nyambu anasema ”Tunaamini tunao wachezaji wazuri kuliko msimu uliyopita ambapo raundi hii tumepania kupambana kwa udi na uvumba kuhakikisha tunaibuka kati ya nafasi sita bora.”

KIPUTE CHA AFRIKA

Prisons Mombasa wakati iliwahi kufanya vizuri ilikuwa mwaka 2014 ilipoibuka ya sita katika jedwali la kipute hicho kilichojumuisha vikosi 14. Hata hivyo kwenye michuano ya muhula uliyopita ulioshirikisha timu 13 kikosi hicho kilimaliza nafasi ya kumi.

Kocha huyo anasema kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo wamepania kujipanga kinoma na kutoa ushindani wa kufa mtu ambapo wamejiwekea azma ya kumaliza kati ya nafasi mbili bora na kutwaa tiketi ya kufuzu kushiriki ngarambe ya Klabu Bingwa Afrika (CAVB).

Anadokeza kuwa Kenya General Service Unit (GSU), Kenya Prisons sio spesheli sana kuwa nyakati zote ndizo hushiriki kipute hicho. ”Kiukweli nasi pia tunamatani sana kushiriki voliboli ya ngarambe hiyo. Sina shaka kutaja kuwa tuna vijana wenye uwezo wa kukabili wapinzani wetu na kufanya kweli kwenye mechi za ligi hapa nchini na kunasa tiketi ya kucheza kipute hicho,” akasema.

Timu ya Prisons Mombasa…Picha/JOHN KIMWERE

MARA TATU

Prisons Mombasa inajivunia mchezaji wake, Jimmy Ngala kuitwa katika kambi ya kikosi cha taifa mara tatu ingawa hakuwahi kuteuliwa katika timu ya mwisho. Naibu kocha Donald Mchete anasema ”GSU, Jeshi la Ulinzi (KDF), Kenya Prisons na Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) hufanya vizuri ligini maana hutumia wachezaji ambao ni wafanyi kazi katika vitengo hivyo.”

Katika mpango mzima vikosi hivyo pia huchangia wana dhoruba wengi kwa timu ya taifa. ”Anakiri kuwa wanafahamu hakuna mteremko kwenye kampeni za muhula huu hasa kwa kuzingatia wapinzani wao waliomaliza kati ya nafasi tano bora msimu uliyopita tayari wameanza kampeni zao kwa kasi,” akasema.

KUMBI ZA NDANI

Aidha anataka Shirikisho la Voliboli la Kenya (KVF) lishirikiane na serikali kwenye juhudi za kuboresha mchezo huo nchini. Anashikilia kuwa ushirikiano wa KVF na serikali unastahili kuhakikisha kumbi za ndani zimejengwa katika maeneo tofauti hasa katika miji mikuu kote nchini. ”

Ni jambo lisilofaa maana hapa nchini timu zetu hufanyia mazoezi kwenye viwanja vya wazi (nje) lakini kwenye mechi za kimataifa huchezea katika kumbi za ndani,” akasema na kuongeza kuwa hatua hiyo huchangia vikosi vya Kenya kutoandikisha matokeo mema.

Baada ya kushiriki patashika mbili Prisons Mombasa chini ya nahodha, Jimmy Ngala imekamata nafasi ya tisa kwa alama tatu, moja mbele ya Trail Blazer sawa na Prisons Western na Equity Bank tofauti ikiwa idadi ya seti. Nahodha huyu anashikilia kuwa dosari ya kikosi chao ni mapokezi ya mipira suala wanalopania kulifanyia kazi ili kupaisha mchezo wao. ”Pia ninaamini nidhamu nzuri italeta matokeo mazuri michezoni,” akasema.

Prisons Mombasa imejumuisha: Nickson Choga, Erick Mambo, Kevin Kipchumba, Jimmy Ngala (nahodha), Richard Amtalla, Dalmas Mukhwana, Nicholas Maina, Philip Chemwor, Baraka Komu, Paul Muhia, Hiram King’ori, Reuben Cheruiyot na Walter Kibet.

Timu ya Prisons Mombasa…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Macho kwa Obiri akiendea mamilioni ya fedha Ras Al Khaimah...

Mkuu wa shule wanafunzi walishambuliwa na magaidi kukamatwa

T L