• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
PSG kuweka mezani Sh13 bilioni kwa ajili ya Richarlson iwapo Mbappe atayoyomea Real Madrid

PSG kuweka mezani Sh13 bilioni kwa ajili ya Richarlson iwapo Mbappe atayoyomea Real Madrid

Na MASHIRIKA

PARIS Saint-Germain (PSG) wamefichua mpango wa kumsajili fowadi matata wa Everton na timu ya taifa ya Brazil, Richarlson Andrade kwa kima cha Sh13 bilioni iwapo Mfaransa Kylian Mbappe, 22, atayoyomea Uhispania kuvalia jezi za Real Madrid.

Iwapo juhudi zao za kumshawishi Richarlson ambaye ni mshambuliaji wa zamani wa Watford kujiunga nao zitaambulia patupu, PSG wameshikilia kwamba watamwendea mfumaji wa Manchester City, Gabriel Jesus ambaye pia ni raia wa Brazil.

Kwa mujibu wa gazeti la L’Equipe nchini Ufaransa, mwanasoka mwingine ambaye PSG wanahisi kwamba ana uwezo wa kujaza kikamilifu pengo la Mbappe ni chipukizi mahiri raia wa Norway, Erling Braut Haaland, 21, ambaye kwa sasa anachezea Borussia Dortmund ya Ujerumani.

Chini ya kocha Rafael Benitez, Everton wameanza tayari kuzungumzia Celtic kuhusu uwezekano wa kumsajili mshambuliaji Odsonne Edouard, 23, ili kujaza pengo litakaloachwa na Richarlson iwapo atahiari kutua PSG baada ya Mbappe kujiengua.

Ili kumdumisha Mbappe uwanjani Santiago Bernabeu, Real watalazimika kutia mnadani wanasoka watatu akiwemo kiungo mvamizi na nahodha wa zamani wa Chelsea, Eden Hazard anayehemewa pakubwa na Juventus ya Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Juventus wanatafuta fowadi atakayejaza pengo la Cristiano Ronaldo ambaye sasa amerejea kambini mwa Manchester United ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Wachezaji wengine watakaoagana na Real ni Marco Asensio, 25, na fowadi chipukizi raia wa Brazil, Rodrygo, 20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Umuhimu wa vitamini E

Montreal yanufaika na kadi nyekundu aliyoonyeshwa Noble...