• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 7:02 PM
Messi afunga mabao mawili na kusaidia PSG kutoka nyuma na kuzamisha RB Leipzig kwenye UEFA

Messi afunga mabao mawili na kusaidia PSG kutoka nyuma na kuzamisha RB Leipzig kwenye UEFA

Na MASHIRIKA

LIONEL Messi alifunga mabao mawili na kusaidia waajiri wake Paris Saint-Germain (PSG) kutoka nyuma na kuzamisha chombo cha RB Leipzig ya Ujerumani 3-2 katika mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku ugani Parc des Princes, Ufaransa.

Kylian Mbappe aliwaweka PSG kifua mbele katika dakika ya tisa kupitia mpira wa kushtukiza. Hata hivyo, juhudi zake zilifutwa na Andre Silva aliyesawazishia Leipzig katika dakika ya 28 kabla ya Nordi Mukiele kuwaweka wageni uongozini kunako dakika ya 57.

Mabao yote ya Leipzig yalichangiwa na kiungo Angelino Tasende. Messi aliwarejesha PSG mchezoni kwa kusawazisha mambo katika dakika ya 67 kabla ya kufunga bao la ushindi dakika saba baadaye kupitia mkwaju wa penalti.

PSG walipata mkwaju mwingine wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili. Lakini badala ya Messi kuchukua fursa hiyo na kufunga bao la tatu, alimwachia Mbappe aliyepaisha mpira juu ya mwamba wa lango la Leipzig.

Mbappe aliyekuwa amefungia PSG penalti 11 za awali, alisema alimweleza Messi apige penalti ya kwanza na amwachie ya pili iwapo ingepatikana.

“Kupoteza penalti ni kawaida kwa mchezaji yeyote. Nilimweleza apige mkwaju wa kwanza na aniachie wa pili. Hiyo ndiyo heshima,” akasema mshambuliaji huyo raia wa Ufaransa.

“Ndiye mwanasoka bora duniani. Ni tija na fahari tele kucheza naye katika kikosi kimoja ndani ya uwanja mmoja. Penalti ya kwanza ilipatikana nikamweleza aipige na nikamwomba aniachie ya pili japo nilipoteza,” akaongeza.

PSG kwa sasa wanaselelea kileleni mwa Kundi A kwa alama saba, moja zaidi kuliko miamba wa Uingereza, Manchester City waliopepeta Club Brugge ya Ubelgiji 5-1 katika mechi nyingine ya UEFA mnamo Jumanne usiku.

Mabao matatu ya Messi tangu ajiunge na PSG muhula huu baada ya kuagana na Barcelona yametokana na mechi za UEFA. Nyota huyo raia wa Argentina aliwahi kufunga goli jingine katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na waajiri wake dhidi ya Man-City katika mechi ya pili ya UEFA kwenye Kundi A.

Messi, 34, sasa anajivunia mabao 123 kutokana na michuano ya UEFA huku Leipzig ikiwa timu ya 37 ambayo Messi ameifunga katika historia ya kipute hicho.

Ndiye mchezaji wa nne baada ya Neymar, Alex na George Weah kuwahi kufunga bao katika mechi mbili za kwanza za nyumbani kwenye UEFA akivalia jezi za PSG.

Chini ya kocha Mauricio Pochettino, PSG walisuasua pakubwa katika mechi hiyo dhidi ya Leipzig huku wakielekezea wapinzani makombora manne pekee yaliyolenga shabaha. Tatu kati ya fataki hizo zilitoka kwa Messi.

Leipzig ambao sasa wamepoteza mechi zote za UEFA msimu huu sasa wanavuta mkia wa Kundi A bila alama. Kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) kimeshinda mechi moja pekee kutokana na nne zilizopita kwenye mashindano yote tangu mikoba yao ianze kudhibitiwa na kocha Jesse Marsch aliyemrithi Julian Nagelsmann aliyeyoyomea Bayern Munich.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

NASAHA: Kufeli kunapaswa kukupa nguvu mpya badala ya...

Refarii Omagwa ajiwekea malengo ya kufika mbali katika soka

T L