• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 12:18 PM
Red Carpet, Uthiru, WYSA zasonga mbele Tim Wanyonyi Super Cup

Red Carpet, Uthiru, WYSA zasonga mbele Tim Wanyonyi Super Cup

Na JOHN KIMWERE

RED CARPET FC imenyuka Kabete Boys mabao 5-2 kwenye mechi ya kuwania taji la Tim Wanyonyi Super Cup 2021 uliopigiwa ugani Kihumbu-ini Kangemi, Nairobi.

Nayo Young Boys ilizaba Big Hawks mabao 7-0.

Young City ilituzwa ushindi wa mezani baada ya Kangemi FC kuingia mitini.

Baadhi ya wachezaji wa Young City baada ya kuzoa ushindi wa mezani dhidi ya Kangemi FC. PICHA | JOHN KIMWERE

WYSA FC ilipiga White Eagles kwa mabao 4-3 baada ya sare ya 2-2, Uthiru Vision ilizima Lucky Boys kwa kuitandika mabao 4-2 huku mabingwa watetezi, Leads United wakisajili ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kibagare Sportiff.

Red Carpet ilipata ufanisi huo kupitia Patrick Otieno na Anthony Ochieng kila mmoja alicheka na wavu mara mbili huku Francis Mmani akifunga bao moja.

Nao Martin Maina na Shadrack Oloo kila moja alifungia kabete Boys bao moja. Bao la Leads ya kocha, Wilston Issa lilitupiwa kimiani na Michael Onyango.

Wenzao wa Young Boys walitesa wapinzani wao na kubeba alama zote tatu kupitia juhudi zao Brian Omondi (mabao manne), Stephen Aungo, Tony Ouko na Elvis Kwateta kila mmoja alitikisa wavu mara moja.

Kwenye mfululizo wa matokeo hayo, Red Carpet Legends ilibanduliwa kwenye kipute hicho ilipozabwa mabao 3-0 na Kangemi Allstars, Wazoefu FC ilikomoa Lopez FC kwa mabao 5-0 nao wanasoka wa Gachie Youth walikung’utwa mabao 4-1 na Kangemi Athletico FC.

”Ninashukuru vijana wangu kwa kazi nzuri waliofanya kwenye mchezo huo,” kocha wa Red Carpet, Meshack Osero alisema na kuongeza kuwa wamepania kujituma kwa udi na uvumba kukabili wapinzani wao Uthiru Vision kwenye mchezo ujao.

Naye kocha wa Leads anasema: ”Tunafuraha tunasonga mbele ambapo tunatarajia kuendeleza mtindo huo kwenye mchezo ujao dhidi ya Ngamia One.”

Ngamia One FC ilijikatia tiketi ya patashika hiyo ilipochapa Pentagon FC 1-0.

Wachezaji wa Pentagon FC. PICHA | JOHN KIMWERE

Leads inajivunia huduma za wachezaji wepesi akiwamo Kelvin Juma, Herman Ngala, Benito Kambele, Bernard Odhiambo, Michael Onyango na Calvin Odhiambo kati ya wengine

Ngarambe ya muhula huu inajumuisha vikosi vikali ikiwamo Leads United na 360 Media FC kati ya timu nyingine.

 

You can share this post!

Oboya Cup: Susa, Rongai zatua nusu fainali

Oboya Cup: Susa, Rongai zatua nusu fainali

T L