• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 8:09 PM
Refa Mary Njoroge kusimamia mchuano wa Argentina dhidi ya Uswidi

Refa Mary Njoroge kusimamia mchuano wa Argentina dhidi ya Uswidi

NA TOTO AREGE

MWAMUZI wa mechi za Shirikiso la Soka Duniani (FIFA) Mary Njoroge, atakuwa mmoja wa marefa katika mechi ya Kundi G ya Kombe la Dunia la Wanawake 2023 kati ya Argentina na Uswidi katika uwanja wa Waikato, Hamilton nchini New Zealand mnamo Jumatano.

Makala ya mwaka 2023 ya Kombe la Dunia la Wanawake, ni yake ya pili kuchezesha, na ni Mkenya pekee anayesimamia michezo hiyo.

Atakuwa mwamuzi msaidizi wa pili katika mechi hiyo ambapo raia wa Rwanda Salima Mukansanga atakuwa mwamuzi wa kati.

Victoire Queency wa Mauritius na Yu-jeong Kim wa Korea watakuwa waamuzi wa kwanza na mwamuzi wa nne mtawalia.

Baada ya mechi mbili za hatua ya makundi, Uswidi wanaongoza kwenye kundi hilo na alama sita.

Italia wanashikilia nafasi ya pili na alama tatu. Nao Afrika Kusini na Argentina wameshikilia nafasi ya tatu na nne wakiwa na alama moja kila moja.

Njoroge alichezesha mechi yake ya kwanza ya mashindano hayo ya Kundi E kati ya Ureno na Vietnam katika uwanja uo huo Alhamisi iliyopita.

Mkenya huyo pia alikuwa mwamuzi msaidizi wa Mukasanga katika Kombe la Dunia la Ufaransa U-20 2018, Kombe la Dunia la Ufaransa 2019 na Mashindano ya Soka ya Olimpiki ya Tokyo 2020.

Ni kwa mara ya kwanza jumla ya timu 32 zinashiriki michuano hiyo kutoka 24 za awali.

Jumla ya waamuzi 33, waamuzi wasaidizi 55 walichaguliwa kutoka katika vyama sita vya Fifa. Afrika ilikuwa na waamuzi wa kati wanne pekee akiwemo Mukasanga. Wengine ni; Vincentia Amedome (Togo), Bouchra Karboubi (Morocco) na Akhona Makalima (Afrika Kusini).

Waamuzi wengine wasaidizi wa Afrika ni pamoja na Carine Atezambong Fomo (Cameroon), Diana Chikotesha (Zambia), Soukaina Hamdi (Morocco), Fatiha Jermoumi (Morocco), Fanta Kone (Mali) na Queency Victoire (Mauritius).

Fainali itafanyika Agosti 20, 2023 katika uwanja wa Accor mjini Sydney.

FIFA ilikuwa iliteua waamuzi 19 wasaidizi wa video (VAR) kwa mara ya kwanza katika Kombe la Dunia la Wanawake huku sita kati yao wakiwa ni wanawake. Adil Zourak kutoka Morocco ndiye mwakilishi pekee wa kiume kutoka Afrika.

  • Tags

You can share this post!

Mswada walenga kuzima waajiri kuhamisha wafanyakazi ghafla

Shakahola: Awamu ya nne ya upasuaji wa maiti yakamilika

T L